Burundi yatuhumiwa kuwakandamiza wapinzani
17 Aprili 2018Tangu Desemba 12 wakati rais Pierre Nkurunziza alipotangaza kufanyika kura ya maoni, maafisa wa serikali na wanachama wa kundi la Imbonerakure yani „wale wanaoona kutoka mbali" wametumia vitisho na ukandamizaji kuhakikisha kura zinaelekezwa kumfaidisha rais Nkurunziza. Kura hiyo itamuwezesha rais huyo wa Burundi ambaye tayari anatumikia muhula uliyo na utata, kuurefusha utawala wake hadi mwaka 2034.
Mateso haya yanajumuisha kumpiga na kumuua mtu mmoja aliyekosa kuthibitisha kuwa amejisajili kupiga kura, kuuwawa kwa watu waliyozuiliwa na polisi pamoja na kamata kamata inayoendelea hasa kwa wanachama wa chama cha upinzani cha National Liberation Forces (FNL).
Aidha duru za kuaminika zimeliambia shirika la Human Rights Watch kwamba visa hivyo vya udhalilishaji vimekuwa vikiendelea nchi nzima. Mnamo Januari 18 muungano wa kisiasa unaojulikana kama Amizero y‘ Abarundi (Matumaini ya Warundi) unaojumuisha wanachama wa kundi la upinzani la FNL ulitangaza kuwa wanachama wake 42 wamekamatwa kiholela tangu Desemba 12.
Hata hivyo imekuwa vigumu kuthibitisha au kupata maelezo zaidi juu ya unyanyasaji unaoendelea kutokana na hofu ya kupata mateso zaidi. Tangu mwaka 2015 wakati mgoggoro wa kisiasa ulipoanza nchini Burundi, baada ya rais Nkurunziza kutangaza kuwania muhula mwengine madarakani, chombo huru cha habari nchini humo na mashirika yasio ya kiserikali vimefungiwa huku zaidi ya watu 397,000 wakiitoroka nchi hiyo, lilisema shirika la Human Rights Watch.
Serikali imetakiwa kusimamisha mara moja visa vya uhalifu nchini Burundi
Akisimulia yaliyomkuta, mkulima mmoja aliye na miaka 20 na mwanachama wa chama cha FNL, anasema alikuwa katika mkahawa mmoja na rafiki yake wakizungumza namna watakavyopiga kura ya hapana katika kura ya maoni, mwanachama wa Imbonerakure aliyekuwepo akawasikia baadaye aliwaita wenzake wakampiga mkulima huyo na mwenzake kabla ya kuwapeleka korokoroni walikozuiliwa huko kwa siku 15.
Aidha serikali imekuwa wazi kwamba itamuadhibu yeyote aliyekuwa na nia ya kusambaratisha kura ya maoni. Msemaji wa wizara ya usalama Pierre Nkurikiye alisema hadharani kwamba kufuatia kamatakamata iliyokuwa ikiendelea ya wale wanaowazuwiya watu kujisajili ni onyo kwa atakaye haribu mchakato wa kura ya maoni. Maafisa wa serikali pia wamesikika wazi wakiwahimiza warundi kupiga kura ya ndio.
Shirika la Human Rights Watch kwa sasa limeitaka serikali ya Burundi mara moja kulizuwia kundi la Imbonerakure kuwahangaisha raia wa taifa hilo, huku wakitaka mfumo wa sheria kuchunguza uhalifu unaoendelea na watakaopatikana na hatia kuhukumiwa.
Serikali pia imetakiwa kuwaamuru polisi kuondoa vitalu vya barabarani vilivyowekwa na kundi hilo la Imbonerakure katika maeneo mbali mbali nchini humo.
Mwandishi: Amina Abubakar/Human Rights Watch
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman