1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la fedha la IMF latakiwa kuifanyia mageuzi bodi yake

Josephat Nyiro Charo29 Septemba 2010

Wanauchumi 13 maarufu na wataalamu wa masuala ya maendeleo duniani Jumanne wiki hii wametoa mwito bodi ya utawala ya shirika la fedha la kimatiafa, IMF, ifanyiwe mageuzi makubwa

https://p.dw.com/p/PQ05
Mkurugenzi mtendaji wa IMF, Dominique Strauss-KahnPicha: AP

Katika barua yao kwa magavana wa bodi ya shirika hilo, watalaamu hao wamegusia wito wa utawala wa rais wa Marekani Barack Obama kuzitaka nchi za Ulaya Magharibi kupunguza idadi ya viongozi wake kwenye bodi hiyo ili kuziwezesha nchi zinazoiunukia kiuchumi kuwa na uwakilishi zaidi.

Barua ya wanauchumi na wataalamu wa maendeleo inazitaka nchi zinazoinukia kiuchumi kama vile China, India pamoja na nchi maskini za Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara na maeneo mengine ya dunia, kuwakilishwa zaidi kwenye bodi ya utawala ya shirika la fedha la kimataifa la IMF. Domenico Lombardi, mtaalamu wa taasisi ya Brookings mjini Washington Marekani na taasisi ya Oxford ya sera ya kiuchumi, ambaye ni miongoni mwa waliosaini barua hiyo amesema Ulaya haifanyi juhudi za kutosha kulifanyia mageuzi shirika la IMF kuhusiana na muundo wa bodi yake ya utawala.

Lombardi, ambaye alihudumu kwenye bodi ya IMF kama mjumbe wa Italia kuanzia 2001 hadi 2005 ameliambia shirika la habari la IPS kwamba wanaunga mkono mageuzi ambayo kwa sasa hayako kwenye ajenda ya shirika la IMF wala muungano wa nchi 20 tajiri duniani, G20, lakini wanayoamini kuwa ni muhimu kama vile kuongeza uwazi katika mchakato wa kupitisha maamuzi, mchakato wa kuwachagua viongozi wa bodi ya IMF na kutathminiwa upya asilimia 85 ya wingi mkubwa unaoipa nchi moja kura ya turufu au muungano fulani wa nchi mbalimbali.

Nchi za Ulaya kwa sasa zinashikilia viti 24 kwenye bodi ya utawala ya fuko la fedha la kimataifa, IMF, ambalo kimsingi linawawakilisha wanachama 187. Na ingawa Umoja wa Ulaya unachangia asilimia 20 ya pato jumla la dunia nzima, unashikilia karibu theluthi moja ya mamlaka jumla ya kupiga kura ndani ya bodi hiyo, ikilinganishwa na aslimia 17 inayoshikiliwa na Marekani, au asilimia 3.72 inayoshikiliwa na China.

Mkurugenzi mtandaji wa shirika la IMF, Dominique Strauss Kahn, ameweka hadi Januari mwakani kama tarehe ya mwisho ya kutekeleza mageuzi. Kama tarehe hiyo itapita, wachambuzi wanaamini makubaliano lazima yafikiwe kwenye mkutano wa nchi za G20 utakaofanyika mjini Seoul, Korea Kusini, mwezi Novemba mwaka ujao.

Barua ya wanauchumi na wataalamu wa maendeleo imelipongeza shirika la IMF kwa hatua zake za kukabiliana na msukosuko wa kiuchumi ulioikabili dunia kwa kutoa fedha zaidi kwa wateja wa tabaka la kati na maskini chini ya masharti machache, lakini ikasisitiza kwamba maendeleo yamekuwa ya mwendo wa kinyonga katika kuboresha masuala muhimu ya utawala wa shirika hilo, ambapo uungwaji mkono wa dhati kutoka kwa wanachama ni muhimu.

Barua hiyo imetaka raia wa nchi wanachama waruhusiwe kupata taarifa kuhusu mikutano ya bodi ya IMF na michakato ya kupitisha maamuzi. Wametaka viongozi wa ngazi ya juu wa shirika la IMF na mashirika mengine ya kimataifa, wachaguliwe kwa uwazi bila kikwazo cha uraia wa wale wanaogombania nafasi hizo. Pendekezo hilo linanuiwa kuumaliza utamaduni wa kumchagua raia wa Ulaya kama mkuu wa IMF na raia wa Marekani kama kiongozi wa benki ya dunia.

Mwandishi: Josephat Charo/ IPS

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman