Sudan: Jeshi lashindwa kuwaondoa waandamanaji
15 Aprili 2019Waandamanaji hao wamesimama imara dhidi ya hatua ya jeshi lillojaribu kuondoa vizuizi walivyovuiweka waandamanaji hao, kwa mujibu wa watu walishuhudia wamesema mwishowe wanajeshi walishindwa. Baraza la mpito la kijeshi, lililochukua mamlaka tangu siku ya Alhamisi limeahidi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia katika muda wa miaka miwili ijayo.
Hata hivyo baadhi ya makundi yanayoshiriki kwenye maandamano hayo yanalitaka baraza la kijeshi likabidhi mamlaka kwa raia baada ya baraza hilo kumng'oa madarakani rais Omar al-Bashir. Makundi hayo yamegoma kuondoka mabarabarani. Wakati huo huo, kuna ripoti kwamba wanachama wa chama cha kiongozi aliyoondolewa madrakani Omar al Bashir cha National Congress Party (NCP) wameanza kukamatwa.
Msemaji wa baraza la kijeshi Luteni Jenerali Shamseldin Kibashi, amesema wanachama wa chama cha NCP hawaruhusiwi kushiriki katika mazungumzo juu ya serikali mpito wala hakitaruhusiwa kujiunga na serikali ya mpito ya kiraia na kwamba kiongozi wa kiraia atachaguliwa na vyama vya upinzani.
Msemaji huyo pia amewataka wapinzani waungane na kumteua waziri mkuu. Omar al- Bashir mwenyewe alikamatwa siku ya Alhamisi, baada ya jeshi kumtelekeza kwa miezi kadhaa iliyokumbwa na maandamano ya kuipinga serikali yake.
Jumatatu,balozi wa Uingereza nchini Sudan, Irfan Siddiq, alisema alikutana na naibu mkuu wa baraza la kijeshi na aliomba kupewa taarifa juu ya mahali alipo Omar al Bashir. Balozi Siddiq pia ametaka iundwa haraka serikali ya mpito ya kiraia kupitia mchakato wa uwazi, wa kuaminika na wa kuzijumuisha pande zote.
Watawala wa kijeshi wa Sudan wanakabiliwa na shinikizo kutoka kwa waandamanaji na serikali za Magharibi. Marekani, Uingereza na Norway zimelitaka baraza la kijeshi la Sudan lifanye mazungumzo na pande zote juu ya kutayarisha kipindi cha mpito kuelekea kwenye utawala wa kiraia. Mabalozi wa nchi hizo wameonya dhidi ya matumizi ya nguvu kwa lengo la kuuzima upinzani wa wananchi. Nchi hizo zimesema madai halali ya watu wa Sudan bado hayajatekelezwa.
Vyanzo:/DPA/AFP