1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Kuna kauli zinazokinzana juu ya usitishaji mapigano

Daniel Gakuba
18 Aprili 2023

Nchini Sudan kuna taarifa zinazokinzana juu ya uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa saa 24, kati ya jeshi la na RSF. Maelfu ya wakaazi wa Khartoum wamejifungia majumbani bila mahitaji ya msingi.

https://p.dw.com/p/4QG6p
Themenpaket: Sudan Konflikt
Picha: AFP

Maafisa wawili wa jeshi la Sudan wametoa kauli zinazopingana juu ya uwezekano wa kusitishwa mapigano na RSF ambayo yalianza Jumamosi.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa facebook, msemaji wa jeshi amesema hajui chochote juu ya muafaka wa usitishaji mapigano, unaosemekana kufikiwa kwa msaada wa wapatanishi wa kimataifa.

Soma zaidi: Msafara wa ubalozi wa Marekani washambuliwa Sudan

Afisa huyo amekishutumu kikosi maalumu cha wanamgambo, RSF kujaribu kuyatumia makubaliano hayo kuficha alichokiita ''kipigo kikali'' kinachowakabili wanamgambo hao katika muda wa saa chache zijazo.

Mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan
Kiongozi wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-BurhanPicha: Uncredited /ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Afueni kwa sababu za kibinadamu

Lakini kabla ya ujumbe huo kuwekwa, jenerali mmoja wa jeshi kwa jina la Shams el Din Kabbashi amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema jeshi liko tayari kwa usitishwaji huo wa mapigano.

''Tumepokea pendekezo kutoka Umoja wa Mataifaa, nchi rafiki na pia waziri wa mambo ya nje wa Marekani, kutaka usitishaji mapigano wa saa 24,'' amesema jenerali Kabbashi, na kuongeza kuwa wamekubali saa 24 tu kwa sababu hali ya kiutu ni mbaya na wakaazi wa Khartoum wanapata tabu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, na hospitali zinakabiliwa na uhaba wa umeme na maji.

''Tunataka muda huu wa saa 24 kuruhusu raia kutembea, na kwa taasisi za serikali kupata mahitaji muhimu,'' ameongeza.

Soma zaidi: Umoja wa Afrika wakutana kuijadili Sudan

Hata kamanda mkuu wa majeshi ya Sudan Abdel Fattah al-Burhan amekiambia kituo cha televisheni cha CNN kuwa yuko tayari kwa muda huo wa ahueni uliopendekezwa na jumuiya ya kimataifa.

Sudan Khartum 2022 | Mohamed Hamdan Dagalo, stellvertretender Vorsitzender Transitional Sovereignty Council
Mohammed Hamdan DagaloPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Afisa mwingine wa ngazi ya juu ameijulisha televisheni ya al-Arabiya kuwa usitishaji huo wa mapigano wa saa 24 ungeanza jioni ya leo Jumanne.

Mkuu wa RSF atuma ujumbe mchanganyiko

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa twitter, kiongozi wa kikosi maalumu cha wanamgambo, RSF Mohammed Hamdan Daglo vile vile ameashiria utayari wake kwa muafaka wa ahueni ya 24 ili kuruhusu raia kuondoka mafichoni na kupeleka hospitalini waliojeruhiwa. Hata hivyo, baada ameandika katika ukurasa huo huo kuwa jeshi limeshindwa kuheshimu ahadi yake. Jenerali al-Burhani alikuwa ahajajibu madai hayo ya Dagalo.

Mapema leo shirika la Msalaba Mwekundu na shirika la Afya ulimwenguni WHO yalikuwa yametowa mwito kwa pande zinazopigana kuruhusu wafanyakazi wa msaada kuwafikia wenye mahitaji, huku idadi ya waliouawa katika makabiliano hayo ikikaribia watu 200.

Chanzo: DPAE, RTRE