1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yajiandaa kuelekea utawala wa kiraia

Angela Mdungu
16 Agosti 2019

Watawala wa kijeshi wa Sudan, na viongozi wa waandamanaji wanatarajiwa kutia sahihi makubaliano yatakayotoa mwongozo kuelekea utawala wa kiraia siku ya Jumamosi.

https://p.dw.com/p/3O0bw
Sudan Abkommen - Ahmed Rabie und General Mohamed Hamdan Daglo
Picha: AFP/A. Shazly

Hatua hii imefikiwa baada ya maandamano ya raia nchini humo yaliyokumbwa na umwagaji damu. Hafla ya utiaji sahihi, itarasimisha azimio la kikatiba lililotiwa saini Agosti 4 kati ya  baraza la mpito la kijeshi na muungano wa  vyama vya upinzani. Makubaliano kati ya pande hizo mbili yamefikisha kikomo miezi minane ya machafuko ambapo raia wengi waliandamana dhidi ya Rais wa zamani wa Sudan Omar Hassan Al Bashir aliyeondolewa madarakani baada ya kutawala kwa miaka 30. 

Makubaliano hayo yalifanyika chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika na Ethiopia na yalipokelewa vyema na pande zote mbili huku waandamanaji wakishangilia kile walichokiona kama ushindi wa mapinduzi yao wakati majenerali wakifurahia kuepusha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wakati maelewano hayo yamefanikiwa kutimiza matakwa kadhaa ya waandamanaji, masharti ya makubaliano yanalipa jeshi madaraka makubwa na kusababisha serikali ijayo ya kiraia ikikabiliwa na changamoto. 

Kutiwa saini kwa nyaraka za makubaliano ya kipindi cha mpito kutaifanya Sudan kuanza hatua ambayo inahusisha hatua muhimu za mwanzo. Muundo wa baraza jipya la mpito lenye raia wengi linatarajiwa kutangazwa Jumapili na siku mbili baadaye litatangazwa jina la waziri mkuu. Hafla ya kutia saini siku ya Jumamosi, haitahudhuriwa na makundi kadhaa ya waasi kutoka maeneo yaliyotengwa kama vile Darfur, Blue Nile na Kordofan Kusini

Abdalla Hamdok kuwa waziri mkuu wa uongozi mpya Sudan?

Siku ya Alhamisi, viongozi wa waandamanaji walikubaliana kumpendekeza Afisa wa zamani wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa Abdalla Hamdok kuwa waziri mkuu. Mchumi huyo mkongwe ambaye aliondoka katika wadhifa wake kama msaidizi wa mkurugenzi mkuu wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika, anatarajiwa kuchaguliwa rasmi ifikapo Agosti 20.

Baraza la mawaziri linatarajiwa kutangazwa Agosti 28, na Waziri Mkuu mpya anatarajiwa kukutana na baraza huru Septemba 1 kwa mara ya kwanza.  Uchaguzi mkuu uni lazima ufanyike baada ya miezi 39 ya kipindi cha mpito ambacho kilishaanza Agosti 4.

Omar Hassan al-Bashir Präsident Sudan Besuch in Libyen
Rais wa zamani wa Sudan Omar Hassan al-Bashir Picha: picture-alliance/dpa

Hadi hapo, nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 40 itakuwa chini ya utawala wa wajumbe 11 wabaraza huru  na serikali ambayo makubaliano yanaweka wazi kuwa itapendekezwa na wananchi. Hata hivyo, mawaziri wa ulinzi na wa mambo ya ndani, watachaguliwa na wajumbe wanajeshi wa baraza. Hatua kuelekea utawala wa kiraia kunaweza kuondoa adhabu ya kuisimamisha Sudan uanachama baada ya maandamano ya mwezi Juni yaliyosababisha umwagaji damu mjini Khartoum.

Bunge linatarajiwa kuundwa ndani ya miezi mitatu na angalau asilimia 40 ya wabunge watakuwa ni wanawake hii ikiwa ni kuakisi kazi kubwa waliyoifanya wanawake katika harakati za maandamano. Vikosi vya kijeshi na taasisi za kijasusi zilizolaumiwa kwa unyanyasaji chini ya utawala wa wa zamani wa Omar al Bashir dhidi ya waandamanani zitafikishwa mbele ya mamlaka ya jeshi na baraza huru la mpito.

Pamoja na hayo, huku mambo mengi yakiwa hayajashughulikiwa, waangalizi wanaonya kuwa ni mapema mno kusema kuwa matukio ya hivi karibuni ni mafanikio katika  mabadiliko ya uongozi. Mmoja wa wanazuoni kutoka Uingereza Rosalind Marsden anasema mabadiliko katika siasa ndiyo yatakayozungumza zaidi na si makubaliano ya kwenye makaratasi