TAMWA: Miaka 36 ya utetezi wa waandishi habari wanawake
29 Novemba 2023Chama hicho kinasema wakati kinaadhimisha miaka 36 ya kuwepo kwake nchini, kinaona kimepiga hatua kubwa katika kuwapigania waandishi wa habari wanawake waliopitia madhila makubwa ikiwamo kukumbana na vikwazo vya kiuchumi na kijinsia.
Kumkomboa mwanamke kutoka daraja la chini, kupigania usawa wa watoto wa kike na mpaka kuwajengea uwezo waandishi wa habari wanawake kushika nafasi za uongozi katika vyombo vya habari, ni baadhi ya mambo ambayo chama hicho kinayataja kuvivunia.
Soma pia:TAMWA yazungumzia rushwa ya ngono kwa wanahabari wa kike
Kikianzishwa mnamo mwaka 1987 na wanwake 13 TAMWA inajitanabaisha kama daraja siyo tu lililowaleta pamoja waandishi habari wanawake kote nchini, bali pia ni chombo kilichofanikiwa kuibua mijadala ya kitaifa na hatimaye kuwezesha mabadiliko ya baadhi ya sera na sheria zilizosaidia kuleta usawa wa kijinsia.
Mwenyekiti wa TAMWA, Joyce Shebe amesema anaona kwamba haya ni mafanikio makubwa hasa kwa kuzingatia historia ya uanzishwaji wake uliokuwa umegubigwa na mifumo dume mingi."Taarifa nyingi za changamoto za wanawake zinaandikwa na zinafuatiliwa ama kutatuliwa."
Mijadala juu ya hali ya uandishi habari
Maadhimisho haya yamekuwa kama sehemu ya ukumbi wa kuibua mijadala kuhusu hali ya uandishi wa habari nchini hasa wakati huu ambako vyombo vya habari vya jadi vinaonekana kuzidiwa nguvu na ujio mpya wa mitandao ya kijamii.
Soma pia: TAMWA yaadhimisha miaka 36 tangu kuasisiwa
Akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho haya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema anatambua mchango unaotolewa na waandishi wa habari wanawake.
"Waandishi wanawake katika taifa la Tanzania na jinsi walivyofanya kazi nzuri sana ya kukomboa wanawake na watoto," alisema waziri Mhagama, ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Mwakilishi wa ubalozi wa Marekani nchini, Jean Clark amesisitiza umuhimu wa kuwa na jamii inayojali na kuheshimu uhuru wa vyombo vya hahari akisema Marekani daima itaendelea kuunga mkono juhudi ya zinazojipambanua kutetea makundi yanayowekwa pembeni.
Ripoti iliyozinduliwa sambamba na maadhimisho hayo, licha ya kutaja maendeleo makubwa yaliyopigwa na waandishi wa habari wanawake, imebainisha pia baadhi ya madhila yanayoendelea kuwakabili.
Soma pia: Vyombo vya habari Tanzania vyatakiwa kupinga rushwa ya ngono
Rose Marandu kutoka mfuko wa ufadhili kwa masuala ya wanawake yaani Women Fund Tanzania, anasema rushwa ya ngono bado inaendelea kuwa donda ndugu linalowaandama waandishi wa habari wanawake chipukizi.
"Wanaoanza kazi kwenye vyombo vya habari ndani ya vyumba vya habari rushwa ya ngono bado ni kubwa sana."
Tamwa inaamini kwamba kwa maadhimisho hayo inapeleka ujumbe kwa jamii jinsi ilivyoanzisha safari ya kupigania haki za wanawake kuanzia maeneo ya kazi mpaka katika maeneo ya maisha ya kawaida.