1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiTanzania

Tanzania yatenga ardhi kwa Zambia kujenga bandari kavu

25 Oktoba 2023

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ametenga ardhi ya hekta 20 kwa jirani yake Zambia ili kujenga bandari kavu, hatua ambayo imetajwa ni mkakati wa kufufua mazingira ya kibiashara na usafiri wa reli.

https://p.dw.com/p/4Y0d9
Rais wa Zambia Hakainde Hichilema
Rais wa Zambia Hakainde HichilemaPicha: picture alliance/dpa/AP

Hatua hiyo imechukuliwa huku utendaji wa reli ya Tazara inayomilikiwa na pande zote mbili ikiendelea kuporomoka kwa kiwango kikubwa. 

Rais Samia amesema ametenga zawadi ya hekta 20 kwa wananchi wa Zambia kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu kwa shabaha ya kuharakisha usafirshaji wa mizigo inayopitiabandari ya Dar es salaam na kisha kusafirishwa kwa barabara hadi sehemu mbalimbali nchini Zambia.

Kiwango cha ufanyaji biashara baina ya pande hizo mbili si cha kuvutia licha ya kuwa ni mataifa yenye historia ya muda mrefu tangu enzi za waasisi wake, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Keneth Kaunda.

Soma pia:Zambia yaingia mkataba wa kulipa madeni yake

Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Mapato TRA, zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka uliopita 2022, Tanzania iliingiza nchini bidhaa kutoka Zambia zenye thamani ya dola za Marekani milioni 91, huku kiwango ilichosafirisha kwenda nchini humo kikiwa dola milioni 80.

Wachambuzi wanasema ziara ya Rais Samia nchini humo, pamoja na ajenda nyingine za kidiplomasia imelenga pia kuangazia eneo hilo la uimarishaji wa mafungamano ya kibiashara.

Changamoto za kibiashara kwa mataifa hayo

Licha ya ahadi za mara kwa mara za viongozi wa maeneo ya nchi za kusini mwa Afrika kutaka ulegezaji wa vikwazo katika maeneo ya mipakani, lakini hata hivyo hali bado ni ngumu katika baadhi ya maeneo. 

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu HassanPicha: Presidential Press Service Tanzania

Joseph Ngonyani raia waTanzania ambaye sasa yuko Zambia alikokwenda kusafirisha mzigo wa kibiashara anasema wakati mwingine amekuwa akivunjwa moyo kutokana na urasimu wa mipakani.

Ama licha ya mataifa haya kuunganishwa na usafiri wa reli ya Tazara hata hivyo nyenzo hiyo haijaonekana kuwa kama ufungua kuwezesha kushamiri kwa shughuli za kibiashara.

Soma pia:Tanzania na Zambia kuimarisha uhusiano wa ujirani mwema

Katika kipindi cha mwaka 2022 kiwango cha usafirishaji mizigo kwa kutumia reli hiyo kilishuka kwa asilimia 51.

Kutokana na kuzorota kwa reli hiyo, duru za habari zinasema, China iliyojenga reli hiyo katika miaka 1960 imekuwa ikizishawishi nchi hizo mbili ikubali ombi lake la kutaka kuichukua na kuiendesha hasa ikilenga usafirishaji wa madini ya shaba.