1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubalozi mpya wa Israel wafunguliwa Bahrain

Josephat Charo
5 Septemba 2023

Ubalozi mpya wa israel umefunguliwa nchini Bahrain. Bahrain inaamini mdahalo na suluhisho la kidiplomasia ni muhimu kutanzua migogoro ya kikanda na kimataifa na kuhakikisha haki za watu kuwa na amani.

https://p.dw.com/p/4VxNu
Bahrain | Abdullatif bin Rashid Alzayani und Eli Cohen
Picha: Bahrain Ministry of Foreign Affairs/AA/picture alliance

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel Eli Cohen amefungua ubalozi wa kudumu wa nchi yake nchini Bahran jana Jumatatu. Ubalozi huo umefunguliwa kama sehemu ya ziara yake ya kwanza katike Ufalme huo wa eneo la Ghuba uliosaini mkataba wa kurejesha mahusiano ya kidiplomasia na Israel mnamo 2020.

Akiwa ameandamana na waziri wa mambo ya nje wa Bahrain Abdullatif al-Zayani, Cohen ameufungua ubalozi huo kwenye eneo jipya katika mji mkuu Manama. Ubalozi huo ulikuwa ukiendesha shughuli zake kutoka kwenye ofisi ya muda iliyofunguliwa na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Israel Yair Lapid mnamo 2021.

Wakati wa ziara yake Cohen amefanya mazungumzo na waziri mkuu wa Bahrain mwana mfalme Salman bin Hamad Al Khalifa kuhusu njia za kuimarisha ulinzi, maendeleo na amani.

Mnamo Septemba 2020 chini ya upatanisho wa Marekani, Israel ilisaini mikataba ya kurejesha mahusiano ya kidiplomasia na Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain. Morocco na Sudan baadaye zilitangaza hatua kama hizo. Kabla hapo nchi mbili za kiarabu, Misri na Jordan, zilikuwa na mahusiano na Israel.