1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchafuzi wa hewa kuongezeka tena mwaka huu

4 Novemba 2021

Utafiti mpya umebaini kwamba uchafuzi wa gesi ya kaboni unaotokana na uchomaji wa nishati za visukuku utarejea mwaka huu kwa viwango vya kabla ya janga la COVID-19, huku China ikiwa mchangiaji mkuu.

https://p.dw.com/p/42ZAk
UK Glasgow | Plakat Klimakonferenz COP26
Picha: Alistair Grant/AP Photo/picture alliance

Utafiti mpya wa kisayasi umebaini kwamba uchafuzi wa gesi ya kaboni unaotokana na uchomaji wa nishati za visukuku utarejea mwaka huu kwa viwango vya kabla ya janga la COVID-19 huku China pekee ikichangia karibu theluthi moja ya uchafuzi jumla. Utafiti huu unatolewa wakati wakuu wa mataifa na serikali wakiwa wamekusanyika mjini Glasgow kwa ajili ya mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi, COP26. 

Kwa mujibu wa tathmini ya kila mwaka iliyotolewa wakati mataifa takribani 200 yanayohudhuria mkutano wa COP26 yakipambana kutafuta njia za uchumi usio na kaboni na kuzuwia kitisho cha kuongezeka kwa joto la dunia, uchafuzi unaotokana na gesi na makaa ya mawe utaongezeka zaidi mwaka huu wa 2021 kuliko ulivyoshuka mwaka uliyopita.

Mnamo mwaka 2020, utoaji wa gesi ya kaboni ulishuka kwa tani bilioni 1.9 sawa na asilimia 5.4 wakati ambapo mataifa yalifunga shughuli za kila siku na uchumi kusimama. Sasa ripoti hiyo iliyotolewa na muungano wa kimataifa wa mradi wa kaboni inatabiri kuongezeka kwa utoaji wa gesi hiyo kwa asilimia 4.9 mwaka huu.

Soma Zaidi: Guterres: Iokoweni dunia ama tutaangamia sote

China inaongoza kwa kuchangia uchafuzi huo kwa kuwa taifa hilo linaegemea zaidi vyanzo hivyo vya uchafuzi katika kuendesha mitambo yake ya nishati.

Mexico Präsident Andres Manuel Lopez Obrador
Rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador amewakosoa viongozi wa mataifa makubwa kwa kuongeza uzalishaji wa gesi chafu.Picha: Hector Vivas/Getty Images

Katika hatua nyingine, kutoka Mexico City, rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador amewakosoa washiriki wa mkutano huo wa kilele wa COP26 kwa kile alichokiita undumilakuwili akiwatuhumu kwa kushindwa kuzungumzia chimbuko la mzozo wa kimazingira huku akiangazia usafiri wa ndege binafsi.

Lopez Obrador amewatupia lawama viongozi wa mataifa makubwa kabisa duniani ambayo yanaongeza uzalishaji wa mafuta na wakati huohuo yanafanya mikutano kwa ajili ya kulinda mazingira huku wakuu haohao wakija kwenye mikutano hiyo kwa kutumia ndege binafsi ndege binafsi.

Obrador ambaye hasafiri mara kwa mara, amesema huo ni unafiki na kuna haja sasa ya kupigania kukosekana kwa usawa ulimwenguni na hicho ndicho atakachokizungumza kwenye kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wiki ijayo ambapo Mexico inachukua uenyekiti.

Picture gallery - the world’s most important forests
Eneo la misitu nchini Indonesia. Waziri wa mazingira anasema makubaliano ya kulinda misitu hayatekelezeki nchini humo.Picha: Dita Alangkara/AP Photo/picture alliance

Na huko Jakarta, waziri wa mazingira Siti Nurbaya Bakar amepuuzilia mbali mpango wa kimataifa wa kuondoa tatizo la uharibifu wa misitu alioutaja kama usiofaa na usio sawa siku chache baada ya taifa lake ambalo ni la tatu kwa kuwa na misitu mikubwa ulimwenguni kuwa miongoni mwa mataifa 100 yaliyoahidi kuondoa kabisa tatizo hilo ifikapo mwaka 2030. 

Soma Zaidi:COP26 yaanza kuonyesha mafanikio 

Makubaliano hayo yalifikiwa siku ya Jumatatu kwenye mkutano huo wa COP26. Waziri huyo ambaye pia alihudhuria mkutano huo ameandika kupitia twitter kwamba si sawa kuilazimisha Indonesia kufikia lengo hilo ifikapo mwaka 2030 na kuongeza kuwa maendeleo ya enzi ya rais Joko Widodo hayatakiwi kuzoroteshwa kwa kile kinachotajwa kama usambazaji wa gesi ya ukaa ama uharobifu wa misitu.

Amesema maana ya uharibifu wa misitu ni pana na inatofautiana na kwa maana hiyo si sawa kuiwekea Indonesia viwango vya Ulaya.

Mkutano huo wa mazingira unaendelea hii leo na ajenda kubwa ikiwa ni nishati chafu na safi.

Soma Zaidi: Mkutano wa mazingira wa UN wafunguliwa rasmi Glasgow

Mashirika: AFPE/RTRE/DW