Raia wa Niger wapiga kura kumchagua Rais mpya
21 Februari 2021Mgombea wa chama tawala Mohamed Bazoum anatarajiwa kushinda hasa baada ya kuongoza kwa asilimia 39.3 ya kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Desemba 27. Mpinzani wake ni rais wa zamani wa nchi hiyo Mahamane Ousmane, ambaye kwenye duru ya kwnza alipata asilimia 17% ya kura.
Bazoum, mwenye umri wa miaka 61 ambaye aliwahi kushika nafasi kadhaa za juu pamoja na wizara za mambo ya nje na mambo ya ndani katika serikali inayomaliza muda wake ya rais Mahamadou Issoufou anaungwa mkono na wagombea walioshika nafasi za tatu na wa nne katika duru ya kwanza ya uchaguzi.
Mohamed Bazoum amesema ataendelea na sera za rais anayeondoka Mahamadou Issoufou, zinazotoa kipaumbele katika maswala ya usalama wakati ambapo nchi hiyo inapambana na waasi, na wakati huo huo amesema ataanzisha sera za kuurekebisha uchumi iwapo atachaguliwa.
Mpinzani wake Mahamane Ousmane, mwenye umri wa miaka 71, alikuwa kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Niger aliyeondolewa mamlakani mnamo mwaka 1996, ameahidi kuleta mabadiliko na kukabiliana ufisadi.
Niger, taifa lililo kwenye ukanda wa Sahel lenye takriban watu milioni 24 ni moja wapo kati ya nchi masikini zaidi ulimwenguni, linakabiliwa na ukame na mafuriko yanayoleta uharibifu mkubwa mara kwa mara. Janga la corona limeuathiri uchumi wa nchi hiyo, hasa wakati huu ambapo bei za madini ya Uranium zimeanguka mno. Madini ya Uranium huiletea Niger mapato kutokana na nchi hiyo kusafirisha nje madaini hayo. Hata hivyo Shirika la Fedha la Kimataifa IMF linatarajia uchumi wa Niger kunawiri kwa zaidi ya asilimia 6% mwaka huu baada ya kudidimia kwa asilimia 1.2% mnamo mwaka 2020.
Mchambuzi wa kisiasa aliyepo mjini Niamey, Elhadj Idi Abou amesema idadi ya watakaojitokeza kupiga kura inatarajiwa kuwa kubwa kutokana wingi wa karibu asilimia 70% ya wapiga kura walioshiriki katika duru ya kwanza ya uchaguzi.
CHANZO:RTRE