Uchambuzi: Mashtaka dhidi ya Trump yaibua mengine mapya
5 Aprili 2023Mashtaka yaliyosubiriwa kwa hamu dhidi ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ya madai ya kumlipa mcheza filamu Stormy Daniels pesa ili akae kimya kuhusu mahusiano yake ya kimapenzi yamefichua mengine mapya katika kesi hiyo ambayo waendesha mashtaka wamefanya uchunguzi kwa miaka mitano.
Mnamo Jumanne mwendesha mashtaka wa wilaya ya Manhattan Alvin Bragg, alisema Trump aliandika rekodi za uwongo za kampuni yake ili kuficha ukweli kwamba alimrudishia wakili wake binafsi Michael Cohen kima cha dola $130,000. Hayo yakiwa ni malipo yaliyofanywa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2016 kwa Stormy Daniels, mwanamke aliyedai kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Trump miaka ya awali.
Trump amshambulia kwa maneno mwendesha mashtaka
Kesi hiyo ni ya kwanza katika historia ya Marekani ya rais wa zamani wa nchi hiyo kushtakiwa kwa kosa la jinai.
Kampeni inayoendelea ya Trump kuwania urais mwaka ujao imeongeza uchunguzi wa ziada kwenye kesi hiyo.
Trump na washirika wake katika chama cha Republic wanadai kesi hiyo imechochewa kisiasa
Wachambuzi wa kisheria wanaohusika kwenye kesi hiyo wamesema uzito wa kesi hiyo utategemea Ushahidi ambao haujawekwa wazi.
Akiwa mahakamani siku ya Jumanne ambapo mashtaka dhidi yake yalifunguliwa rasmi, Trump aliyakana madai hayo.
Upotoshaji wa rekodi za biashara huko New York ni makosa, lakini ni hatia ya jinai inapofanywa kwa nia ya kuficha uhalifu mwingine.
Akizungumza na waandishi wa habari, Bragg alisema, njama hiyo ililenga kuficha ukiukwaji wa sheria ya jimbo la New York inayoifanya kuwa uhalifu hatua ya kula njama "kumkuza mgombea kwa njia zisizo halali.
Trump ajitetea, adai Wademocrat waihujumu azma yake ya urais
Alisema malipo ya $130,000 yamevuka kikomo cha shirikisho kwenye michango ya kampeni.
Lakini maelezo kwa undani ya mashtaka yote 34 dhidi ya Trump hayajatolewa, na hatua ya kuyaweka kuwa siri yanawashangaza baadhi ya wachambuzi wa sheria.
Mark Bederow, afisa wa zamani katika ofisi ya mwendesha mashtaka wa Manhattan amesema alikuwa akitarajia kusikia kinagaubaga yaliyomo kwenye mashtaka na jinsi uhalifu huo ulivyofanywa, lakini hilo halijatimia.
Aliyekuwa wakili binafsi wa Trump Michael Cohen alikiri kosa la kukiuka sheria kuhusu fedha za kampeni kufuatia malipo yake kwa Daniels, ingawa Trump hakuwa ameshtakiwa kwa uhalifu wakati huo. Mtangulizi wa Bragg pia alichunguza Kashfa hiyo lakini hakufungua mashtaka.
Haijulikani wazi ni ushahidi wa aina gani, ambao Bragg aliotowa kwa Baraza Kuu la Mahakama ndipo wakaidhinisha kushtakiwa kwa Trump.
Mashtaka yalijikita kwenye malipo kwa njia ya hundi ambazo Trump alimlipa Cohen. Lakini uwasilishaji mwingine wa waendesha mashitaka, unaojulikana kama taarifa ya ukweli, ilielezea mipango ambayo Trump anadaiwa kufanya kuwanyamazisha watu wengine wawili ambao walisema walikuwa na taarifa mbaya kumhusu.
Kulingana na wachambuzi wengine wa sheria, hiyo inaweza kumsaidia mwendesha mashtaka kuthibitishia mahakama kuwa Trump alikusudia kufanya kosa la jinai.
Cohen ambaye aliyesema Trump alimshauri amlipe Stomy daniels, alitoa ushuhuda mbele ya baraza kuu la mahakama hiyo wiki iliyopita na kumtia Trump hatiani.
Lakini mwaka 2018, Cohen alikiri hatia ya kulidanganya bunge. Vilevile kuhusu ukiukwaji wa fedha za kampeni kutokana na malipo kwa Daniels. Haya yanaweza kumuacha wazi kwa mashambulizi kutoka kwa mawakili wa Trump kuhusu uaminifu wake.
Lakini Jeremy Saland ambaye ni afisa mwengine wa zamani katika ofisi ya mwendesha mashtaka ya Manhattan ametahadharisha kwamba waendesha mashtaka wanafahamu wana safari ndefu kushughulikia mashtaka hayo, ili kuithibitishia mahakama kama kweli Trump alikusudia kukiuka sheria ya uchaguzi, hata ingawa hajashtakiwa kwa kosa hilo.
(Chanzo: RTRE)