1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiBrazil

Uchunguzi unafanyika kutambua wahanga wa ajali ya ndege

11 Agosti 2024

Familia za wahanga wa ajali ya ndege Brazil wamekusanyika leo katika vyumba vya kuhifadhia maiti mjini Sao Paulo wakati wachunguzi wa vinasaba wakijaribu kutambua mabaki ya miili ya watu 62 waliofariki katika ajali hiyo.

https://p.dw.com/p/4jLbq
Passagieren-Flugzeug in Brasilien abgestürzt
Wazima moto na waokoaji wakikagua vifusi baada ya ndege iliyokuwa na watu 61 kuanguka Vinhedo, jimbo la Sao Paulo, Brazil.Picha: Andre Penner/AP Photo/picture alliance

Mamlaka nchini Brazil imesema katika taarifa kuwa mabaki ya wahanga wote wa ajali yamepatikana wakiwemo wanaume 34 na wanawake 28.

Miili ya rubani mkuu Danilo Santos Romano na msaidizi wake Humberto de Campos Alencar e Silva, ilikuwa ya kwanza kutambuliwa na wataalamu hao wa vinasaba.

Soma pia: Brazil yatangaza siku tatu za maombolezo baada ya ajali ya ndege kuuwa watu 61

Ndege chapa ATR 72 yenye injini mbili inayomilikiwa na kampuni ya ndege ya Voepass ilianguka Ijumaa jioni katika mji wa Vinhedo, wakati ikitokea jimbo la kusini la Parana kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sao Paulo.

Mamlaka ya usafiri wa anga nchini humo imesema vifaa vinavyorekodi mwenendo na taarifa za ndege vimetumwa katika maabara ya mji mkuu wa Brasilia kwa uchunguzi zaidi.

Matokeo ya uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo yanatarajiwa kutolewa ndani ya siku 30.