Kongamano la kibinaadamu kwa ajili ya Gaza laanza Ufaransa
9 Novemba 2023Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye ndiye muasisi wa kongamano hilo la kibinaadamu kwa ajili ya msaada zaidi kwa Gaza amesema katika hotuba ya ufunguzi kuwa ni lazima kuwepo haraka usitishwaji wa muda wa mapigano kwa sababu za kiutu. Macron amesema suala lisilo na mjadala ni kwamba ni lazima raia walindwe.
Kabla ya mkutano huo, Macron amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na anatarajia pia kuzungumza naye baadaye. Hata hivyo serikali ya Tel-Aviv haitawakilishwa katika kongamano hilo lililoandaliwa na Ikulu ya Ufaransa ya Elysée.
Licha ya kuwa nchi za kiarabu hazitawakilishwa na viongozi wa ngazi za juu katika mkutano huo, Macron amezungumza pia kwa njia ya simu na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, ambao wamekuwa na jukumu muhimu katika kuwezesha utoaji wa misaada katika Ukanda wa Gaza, ambako wanaishi Wapalestina wapatao milioni 2.4.
Soma pia: Israel inaendeleza mashambulizi yake katika ukanda wa Gaza
Mamlaka ya Palestina imewakilishwa na Waziri Mkuu wake huku Misri ambayo inadhibiti kivuko pekee kisichodhibitiwa na Israel cha Rafah, itautuma ujumbe wa mawaziri mjini Paris. Mkutano huo, hata hivyo, utafuatiliwa kwa karibu na mashirika ya kibinadamu, ambayo yamekuwa yakishutumu kwa nguvu zote idadi ndogo pamoja na shida wanazokabiliana nazo katika utoaji misaada, vinavyotatizwa na mashambulizi yanayoendelea ya Israel kwenye Gaza.
Miito ya usitishwaji mapigano na makadirio ya misaada
Mashirika ya Kimataifa yasio ya kiserikali yapatayo 13 yametoa wito siku ya Jumatano wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuhimiza uheshimishwaji wa sheria za kimataifa kuhusu masuala ya kibinaadamu huku wakisisitiza kuhusu kuwasilishwa kwa msaada huko Gaza.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye amesema, jinamizi la Gaza ni zaidi ya janga la kibinadamu, na sasa ni janga la ubinadamu. Umoja wa Mataifa unakadiria mahitaji ya misaada kwa wakazi wa Gaza na Ukingo wa Magharibi kufikia dola bilioni 1.2 hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023.
Viongozi walio karibu na utawala mjini Paris wamesikika wakisema kwamba ni wazi kwa rais Macron kuwa Israel ina haki ya kujilinda, lakini leo hii, idadi ya wahanga imekuwa kubwa mno huko Gaza.
Malengo ya mkutano huo wa Paris
Mkutano huo unalenga kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu hali halisi ya misaada huko Gaza lakini pia kuhamasisha wadau na wafadhili wote ili kuweza hatimaye kukidhi mahitaji hayo.
Soma pia: Kundi la G7 lasema Israel ina haki ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Hamas
Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, mijadala hiyo itajumuisha sehemu ya misaada ya chakula, vifaa vya matibabu na nishati, suala lenye utata mkubwa, kwa kuwa Israel haitaki mafuta petroli kuingia katika Ukanda wa Gaza wakihofia kuwa yanaweza kutumiwa na Hamas katika harakati zao za kijeshi.
Sehemu ya pili ya mkutano huo itahusu ahadi za michango na kuratibu masuala ya utendaji kuhusu ufikiaji wa misaada ya kibinadamu huko Gaza na Ufaransa imeahidi kuwa itaongeza michango yake ya kifedha kwa ajili ya ukanda wa Gaza ambao umezingirwa na vikosi vya Israel kwa mwezi mmoja sasa.
Kulingana na vyanzo vya kuaminika, hakutakuwa na tamko la pamoja mwishoni mwa mkutano huo ili kuepuka mjadala usio na mwisho na serikali ya Paris imesisitiza kuwa kongamano hilo ni la kibinadamu na kamwe lisiugeuzwe kuwa jukwaa la kuilaani Israel.
Chanzo: (AFP, RTR)