Ufaransa yawaondoa wanajeshi wake wa mwisho Niger
22 Desemba 2023Hatua inayoashiria kumalizika kwa zaidi ya muongo mmoja wa operesheni za Ufaransa dhidi ya wapiganaji wa itikadi kali katika eneo la Sahel. Wakati huo huo Ufaransa nayo imesema itafunga ubalozi wake nchini humo.
Luteni wa jeshi la Niger Salim Ibrahim amesema kwamba tarehe ya leo inaashiria mwisho wa mchakato wa kuondolewa kwa vikosi vya Ufaransa katika eneo la Sahel.
Soma pia: Viongozi wa ECOWAS wakutana kujadili muelekeo wa mataifa yaliyo chini ya utawala wa kijeshi
Ufaransa ilisema itawaondoa wanajeshi wake takriban 1,500 na marubani kutoka Niger baada ya majenerali wapya wa koloni hilo la zamani la Ufaransa kuwataka waondoke kufuatia mapinduzi ya kijeshi mnamo Julai 26.
Hii ni mara ya tatu katika muda wa chini ya miezi 18 kwa wanajeshi wa Ufaransa kutimuliwa katika nchi iliyo kwenye eneo la Sahel.
Wanajeshi wa Ufaransa wamelazimika kuondoka kutoka kwenye nchi zilizokuwa zamani koloni zake kama vile Mali mnamo mwaka jana na Burkina Faso mapema mwaka huu kufuatia mapinduzi ya kijeshi kama ilivyo kwa Niger.
Mataifa yote matatu yanapambana na uasi wa itikadi kali za dini ya kiislamu uliozuka kaskazini mwa Mali mwaka 2012, na baadaye kuenea hadi Niger na Burkina Faso.
Msururu wa mapinduzi katika eneo hilo tangu 2020 umesabaisha kuharibika kwa uhusiano wake na Ufaransa na mwelekeo wake kuegemea zaidi katika maelewano na Urusi.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitangaza mnamo Septemba kuondoa wanajeshi wote wa Ufaransa kutoka Niger ifikapo mwisho wa mwaka, na kikosi cha kwanza kiliondoka mnamo Oktoba.
Soma pia: EU: Yaweka vikwazo kwa utawala wa kijeshi Niger
Hata hivyo kuondoka kwa Ufaransa kunawaacha mamia ya wanajeshi wa Marekani, Italia na Ujerumani.
Ufaransa imejibu
Huku haya yakijiri vyanzo vya kidiplomasia vya Ufaransa vimesema kwamba taifa hilo litafunga ubalozi wake nchini Niger.
Kulingana na vyanzo hivyo vya kidiplomsia kutoka mjini Paris, wanadiplomasia wengi wa Ufaransa walianza kuondoka nchini humo tangu mwisho wa mwezi Septemba baada ya ubalozi huo kushambuliwa na kuwekewa vizuizi.
Vyanzo hivyo vimeeleza kwamba kufuatia mapinduzi ya kijeshi ubalozi haupo tena katika nafasi ya kufanya kazi kama kawaida au hata kutimiza wajibu wake.
Ufaransa, pamoja na nchi nyingine za Magharibi na baadhi ya mataifa ya Afrika, zimekataa kutambua serikali mpya ya kijeshi yaNiger.
Niger, nchi ya Afrika Magharibi isiyo na bandari yenye takriban watu milioni 26 ilikuwa taifa la mwisho lenye utawala wa kidemokrasia kwenye kanda ya Sahel ambalo Ufaransa ilisalia kuwa mshirika wake mkubwa. Utawala uliopinduliwa ulikuwa vilevile na usuhuba na mataifa mengine ya magharibi hususani Marekani katika mapambano dhidi ya ugaidi katika ukanda wa Sahel.