Ufisadi waikumba Ukraine, Ulaya ikizozana kuitumia vifaru
24 Januari 2023Hapo Jumapili, polisi wa kukabiliana na ufisadi nchini Ukraine walisema kwamba wanamshikilia naibu waziri wa miundo msingi kwa madai ya kupokea rushwa ya dola laki nne katika uagizaji wa jenereta kutoka nje ya nchi mwezi Septemba.
Utafiti mmoja wa gazeti pia uliituhumu wizara ya ulinzi kwa kulipa fedha kupita kiasi kwa ajili ya chakula cha wanajeshi. Ukraine ina historia ndefu ya ufisadi na utawala usio thabiti.
Mawaziri na maafisa wengine kuachishwa kazi
Na sasa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema anapanga kukaza kamba katika usafiri wa maafisa wa serikali nje ya nchi kwa ajili ya majukumu rasmi.
Katika ujumbe wake wa video anaoutoa kila usiku, Zelenskiy hapo Jumatatu alisema,
"Tayari kuna maamuzi binafsi, mengine nitayatoa leo mengine kesho, kuhusiana na maafisa wa ngazi tofauti katika wizara na serikali kuu na hata pia katika serikali za majimbo na katika idara ya polisi," alisema Zelenskiy.
Vyombo kadhaa vya habari nchini Ukraine vimeripoti kwamba huenda mawaziri na maafisa waandamizi serikalini huenda wakaachishwa kazi mara moja.
Sakata hili la ufisadi huenda likapelekea nchi za Magharibi kufikiria mara mbili kuhusiana na kuipelekea Ukraine misaada, wakati ambapo kuna vuta ni kuvute miongoni mwa mataifa ya Ulaya kuhusiana na kupeleka nchini humo, vifaru vya kivita kutoka Ujerumani.
Ukraine inasema inavihitaji vifaru hivyo chapa Leopard 2 ili kukabiliana na jeshi la Urusi na kuyarudisha katika himaya yake maeneo yaliyotekwa.
Ujerumani ambayo ni lazima itoe ridhaa ya vifaru hivyo kupelekwa Ukraine, inaonekana kusuasua kwa hofu ya kuichokoza Urusi na kuvizidisha vita hivyo. Lakini Ujerumani imesema iko tayari kuchukua hatua za haraka za kuvituma vifaru hivyo iwapo kutakuwa na maafikiano baina ya nchi marafiki zake.
Mageuzi ya jeshi la Urusi ni kwa ajili ya kukabiliana na vitisho
Wabunge wa Marekani, wameishinikiza serikali yao kupeleka Ukraine, vifaru chapa M1 Abrams, wakisema hata ikitumwa idadi ndogo ya vifaru hivyo, marafiki zake wa Ulaya nao watapata motisha wa kutuma vifaru vyao.
Uingereza imesema itatuma vifaru 14 chapa Challenger 2 nayo Ufaransa imesema haiondoi uwezekano wa kutuma vifaru aina ya Leclerc.
Kwa upande wake Urusi kupitia jenerali mpya aliyeteuliwa kusimamia operesheni za Urusi nchini Ukraine, Valery Gerasimov, amesema mageuzi ya hivi karibuni yaliyofanywa katika jeshi ni kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vinavyotolewa dhidi ya urusi na uwezekano wa Jumuiya ya NATO kupanuka kwa Sweden na Finland kujiunga na jumuiya hiyo.
Gerasimov anasema Urusi haijashuhudia uvamizi wa kijeshi kiasi hiki kutoka nchi za Magharibi na ndilo jambo linaloipelekea kufanya operesheni zake za kijeshi ili kuituliza hali hiyo.
Chanzo: Reuters