1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Uganda yawazuilia waandamanaji kadhaa wanaopinga ufisadi

24 Julai 2024

Watu kadhaa walioshiriki katika maandamano ya kupinga ufisadi katika mji mkuu wa Uganda Kampala kwa kukaidi marufuku ya serikali wameshitakiwa na kuwekwa jela.

https://p.dw.com/p/4ieKR
Maandamano ya kupinga ufisadi Uganda
Polisi walishika doria mjini Kampala na kuweka vizuwizi kwenye barabara za kuelekea bungeniPicha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Mawakili wamesema karibu watu 60, akiwemo mtangazaji maarufu wa televisheni na redio na vijana watatu viongozi wa maandamano, walifikishwa haraka mahakamani na kuwekwa rumande kwa mashitaka yakiwemo "usumbufu wa umma." Polisi wa kukabiliana na vurugu walishika doria kote Kampala, na kuweka vizuwizi barabarani hasa karibu na eneo la kibiashara, huku maafisa wakizifunga barabara za kuelekea bungeni.

Msemaji wa polisi Kituuma Rusoke alisema mamlaka hazitoruhusu maandamano yoyote ambayo yanatishia amani na usalama wa Uganda. Wito wa maandamano ya kupinga ufisadi ulitolewa na vijana wa Uganda kwenye mitandao ya kijamii, wakipata msukumo kutoka kwa maandamano ya vijana wa nchi jirani Kenya maarufu kama Gen-Z.

Soma pia: Wabunge wa upinzani Uganda wafungwa jela kabla ya maandamano ya kupinga rushwa

Rais Yoweri Museveni ambaye ameliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa mkono wa chuma kwa miongo minne, alikuwa ameonya mwishoni mwa wiki kuwa waandamanaji walikuwa "wakicheza na moto."