1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama waimarishwa Kampala kufuatia maandamano ya vijana

23 Julai 2024

Mji wa Kampala umeamkia hali ya taharuki ambapo polisi na majeshi wameweka doria kali kuyadhibiti maandamano ya vijana wanaopinga ufisadi uliokithiri. Wabunge wa upinzani wamesema wanaunga harakati hizo za vijana.

https://p.dw.com/p/4id2X
Uganda Kampala 2024 | Polizei riegelt Parlament vor geplanter Anti-Korruptions-Demonstration ab
Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Vijana waliandamana katika eneo la viwanda wakisema huu ndiyo wakati wa kuleta mabadiliko ili mustakabali wao uwe wa amani. Licha ya onyo kali kutoka kwa vyombo vya usalama pamoja na ushauri wa rais Museveni kwamba maandamano ya vijana maarufu kama Gen Z yafanyike siku ya Jumapili kwenye uwanja wa uhuru wa Kololo, wale waliodai kuongoza maandamano hayo wameshikilia kuwa maandamano yataendelea kama walivyopanga. 

Baada ya kubaini kuwa vijana hao wameshikilia kuendelea na maandamano hayo, vyombo vya usalama vikiongozwa na polisi vimechukua hatua ya kuweka doria kali sehemu zote za mji mkuu wa Kampala. 

Akihutubia taifa mwishoni mwa wiki rais Museveni aliunga mkono maandamano hayo dhidi ya ufisadi ila aliwatakuwa vijana wakubali kufanya maandamano hayo ya amani siku ya Jumapili kwenye uwanja wa sherehe za kitaifa. 

Maandamano haya ya Uganda yanafanyika wakati mmoja na yale ya Kenya ambapo vijana  walitangaza kuendelea na maandamano kumshinikizs rais William Ruto kujiuzulu

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala