Ugiriki yatoa mapendekezo mapya
21 Juni 2015Serikali ya Ugiriki imetoa mapendekezo mapya muda mfupi tu kabla ya mkutano wa viongozi wa Ukanda wa sarafu ya Euro wanaotarajiwa kuutafuta ufumbuzi katika dakika za mwisho ili kuiepusha Ugiriki kufilisika.
Waziri wa nchi wa Ugiriki Alekos Flambouraris amesema kwa kutoa mapendekezo hayo mapya, nchi yake inataka kuyaboresha yale ambayo imeshayatoa hadi sasa. Kwa mujibu wa Waziri huyo, ambae ni mtu wa karibu wa Waziri Mkuu, Alexis Tsipras, tofauti baina ya Ugiriki na wakopeshaji wake sasa siyo kubwa tena.
Hatari ya kufilisika
Pande tatu zilizoikopesha Ugiriki - Umoja wa Ulaya, Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, na Benki Kuu ya Ulaya ECB, zinaitaka nchi hiyo ibane zaidi matumizi, kiasi cha Euro Milioni 450 ili iweze kupatiwa fedha nyingine za msaada, kiasi cha Euro Bilioni 7.2. Fedha hizo zimekuwa zinazuiwa kwa muda wa miezi kadhaa kutokana na tofauti zilizopo juu ya sera ya kubana matumizi baina ya Ugiriki na wadai wake.
Hata hivyo Waziri wa nchi wa Ugiriki Flambouraris amesema nchi yake itawasilisha mapendekezo yenye lengo la kupunguza tofauti na wadai wa Ugiriki.
Waziri huyo pia amearifu kwamba, kutokana na mkwamo unaoendelea na kutokana na hatari ya Ugiriki kufilisika huenda leo Waziri Mkuu wa nchi hiyo Alexis Tsipras akawasiliana na Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker kwa njia simu.
Wakati huo huo Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis ametoa mwito kwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kumtaka autoe uamuzi juu ya Ugiriki. Waziri Varoufakis ameliambia gazeti la Ujerumani "Frankfurter Allgemeine Sontagszeitung" kwamba Kansela Merkel anaweza kufikia mapatano ya taadhima na serikali ya Ugiriki inayojitahidi kuleta suluhisho.
Kwa muda wa miezi kadhaa sasa Ugiriki imekuwa inafanya mazungumzo na wakopeshaji wake juu ya masharti ya kuwezesha kutolewa fedha zaidi kwa ajili ya kuisaidia Ugiriki. Ikiwa makubaliano hayatafikiwa mnamo siku za karibuni,Ugiriki itaweza kufilisika na yumkini ikalazimika kujiondoa kwenye ukanda wa sarafu ya Euro.
Hata hivyo serikali ya Ugiriki inaendelea kushinikizwa ili ichukue hatua zitakazoleta suluhisho la mgogoro wake mkubwa. Waziri wa fedha wa Marekani Jacob Lew amezitaka pande zote ziwe na moyo mnyumbufu ili kuuondoa mkwamo.
Spika wa Bunge la Ulaya Martin Schulz ameionya Ugiriki dhidi ya kujaribu kujiondoa kwenye Ukanda wa sarafu ya Euro, kwa kutumai kupata msaada wa fedha kutoka kwenye mfuko wa Umoja wa Ulaya.
Lakini uwezekano wa Ugiriki kujitoa kwenye sarafu ya Euro umesababisha wananchi wa nchi hiyo wazitoe akiba zao za benki kwa wingi. Mnamo siku chache zilizopita Wagiriki walitoa Euro zaidi ya Bilioni 4 kutoka kwenye akiba zao za benki.
Wajerumani wataka Ugiriki iondoke
Wananchi wa Ujerumani wanakasirishwa na Ugiriki baada ya miezi mitano ya mzungumzo ya kuvutana baina ya serikali ya nchi hiyo na wadai wake. Na kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni asilimia 51 wa Wajerumani sasa wanaamini kwamba Ugiriki inaweza kujiondoa kwenye ukanda wa sarafu ya Euro.
Viongozi wa nchi na wakuu wa serikali wa ukanda wa sarafu ya Euro watakutana JUmatatu mjini Brussels ili kujaribu kuitafuta njia ya kuuondoa mkwamo. Ugiriki inapaswa kulilipa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF kiasi cha Euro Bilioni 1.5 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu.
Mwandishi: Mtullya Abdu /afp,dpa.
Mhariri: Iddi Ssessanga