Uingereza kulipiga marufuku kundi la Wagner
6 Septemba 2023Uingereza inapanga kulipiga marufuku kundi la wapiganaji mamluki la Urusi la Wagner kama shirika la kigaidi. Ripoti hizo zimetolewa na vyombo vya habari vya Uingereza vikimnukuu waziri wa mambo ya ndani Suella Braverman.
Ripoti ya gazeti la Daily Mail imesema Uingereza inajiandaa kuliorodhesha kundi la Wagner kuwa la kigaidi kwa mujibu wa sheria za kupambana na ugaidi na hivyo kuliweka katika ngazi moja na kundi linalojiita Dola la Kiislamu na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda.
Gazeti hilo limemnukuu waziri Braverman akisema kundi la Wagner ni shirika lenye vurugu na uharibifu ambalo limeendesha shughuli zake kama chombo cha kijeshi cha rais wa Urusi Vladimir Putin katika nchi za nje na limehusika katika uporaji, mateso na mauaji ya kinyama.
Waziri huyo pia amesema harakati za kundi hilo nchini Ukraine, Mashariki ya Kati na barani Afrika ni kitisho kwa usalama wa dunia.