Uingereza yalaani uamuzi wa kuzuia wahamiaji kwenda Rwanda
18 Juni 2022Katika mahojiano na gazeti la The Telegraph, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Priti Patel amenukuliwa siku ya Jumamosi akisema kuwa mahakama hiyo ilifanya kazi kwa njia isiyo ya wazi na uamuzi huo ulichochewa kisiasa.
"Unapaswa kuangalia sababu zake," aliiambia The Telegraph, baada ya mahakama hiyo siku ya Jumanne kuizuia dakika za mwisho ndege iliyokuwa na wahamiaji ilipotaka kuondoka kwenda Kigali.
Waziri Patel amesema uamuzi wa mahakama ya ECHR unapaswa kufuatiliwa. Amebainisha kuwa serikali ya Uingereza haikuelezwa kuhusu majina ya majaji wa mahakama hiyo na haikupokea uamuzi kamili wa amri ya kutowahamisha wahamiaji hao hadi mapitio ya sera hiyo yatakapokamilika.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema Jumamosi kuwa ana uhakika na uhalali wa mpango wa serikali yake kuwapeleka nchini Rwanda watu wanaoomba hifadhi, baada ya ndege ya kwanza kuzuiwa katika dakika za mwisho na mahakama ya ECHR. Johnson ameuelezea uamuzi huo kama pigo la ajabu katika dakika za mwisho.
Mahakama Uingereza hazikuwa na pingamizi
"Kila mahakama kwenye nchi hii imesema hapakuwa na kikwazo ambacho wangeweza kukiona, hakuna mahakama kwenye nchi hii iliyotoa uamuzi kuwa sera hiyo ni kinyume cha sheria ambao ulikuwa wa kutia moyo sana," Johnson aliwaambia waandishi habari. Waziri huyo mkuu wa Uingereza amesema wanajiamini katika uhalali wa kile wanachokifanya na wataendelea kuitekeleza sera hiyo.
Kuingilia kati kwa kuchelewa kwa mahakama ya Ulaya kumesababisha baadhi ya wanasiasa kutoka chama cha Kihafidhina cha Waziri Mkuu Boris Johnson kutoa wito kwa Uingereza kujiondoa kabisa katika Mahakama ya Ulaya inayoshughulikia Haki za Binaadamu.
Siku ya Alhamisi, Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Dominic Raab alisema kwamba nchi hiyo haina mpango wa kujiondoa kwenye mahakama ya ECHR, lakini aliongeza kuwa mahakama hiyo iliyoko Strasbourg, imevuka mamlaka yake katika kuzuia uhamishaji huo.
Hata hivyo, Raab amesema hawezi kutangaza tarehe kamili ambayo kundi la kwanza la watu wanaoomba hifadhi litapelekwa Rwanda chini ya mpango wa serikali ya Rwanda wa kuwahamisha wahamiaji.
Uingereza kuimarisha mipaka yake
Serikali ya Uingereza ambayo iliahidi kuimarisha mikapaka yake baada ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, Brexit iko katika shinikizo la kukabiliana na idadi kubwa ya wahamiaji wanaovuka mipaka kupitia bahari kwa kutumia boti ndogo kutoka kaskazini mwa Ufaransa.
Tangu kuanza kwa mwaka huu hadi sasa, zaidi ya watu 11,000 wamezuiwa na kupelekwa kwenye maeneo ya ufukweni, hiyo ikiwa ni karibu mara mbili ya idadi hiyo kwa wakati kama huo katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Lakini mkataba wenye utata uliosainiwa na Rwanda wa kuwapeleka baadhi ya watu wanaoomba hifadhi kwa ajili ya kupata makaazi mapya kwenye nchi hiyo ya Afrika Mashariki, umesababisha gadhabu kubwa.
Takribani wahamiaji 130 walikuwa wamepangiwa kuondoka siku ya Jumanne kwa usafiri wa ndege, lakini idadi hiyo ikapungua hadi sifuri, baada ya kuwekwa kwa vipingamizi kadhaa vya kisheria kwa misingi ya haki za binaadamu.
Serikali ya Uingereza inafikiria kuandika upya Sheria ya Haki za Binaadamu ya Uingereza, ambayo inaitegemea Mahakama ya Ulaya inayoshughulikia Haki za Binaadamu, ili iwe rahisi kwa nchi hiyo kuwaondoa wahamiaji.
Johnson amewakosoa mawakili kwa kushughulikia kesi za watu wanaoomba hifadhi na madai ya Patel kuhusu mwelekeo wa kisiasa kwa uamuzi wa mahakama ya ECHR, yanalingana na maelezo ya serikali kuhusu vitisho kwa uhuru wa Uingereza unaofanywa na taasisi za Ulaya.
Hata hivyo, Mahakama ya Ulaya inayoshughulikia Haki za Binaadamu, sio sehemu ya Umoja wa Ulaya ambayo Uingereza ilijiondoa mwezi Januari mwaka uliopita, na Uingereza ilisaidia katika kuianzisha mahakama hiyo na kuuandaa mkataba huo.
(AFP, Reuters)