1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kujibu haraka kuhusu vifaru vya kivita kwa Ukraine

25 Januari 2023

Ujerumani inatarajiwa kutoa uamuzi leo Jumatano juu ya iwapo vifaru vyake vya kivita aina ya Leopard vinaweza kupelekwa nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4MfYp
Polen Challenger 2 Panzer
Picha: Tomasz Waszczuk/PAP/epa/dpa/picture alliance

Ujerumani inatarajiwa kutoa uamuzi leo Jumatano juu ya iwapo vifaru vyake vya kivita aina ya Leopard vinaweza kupelekwa nchini Ukraine. Nchi za Magharibi zimekuwa zikiahidi silaha zaidi za kijeshi ili kuisaidia Ukraine kupambana na mashambulizi kutoka Urusi.

Ujerumani ilisita kutoa uamuzi huo hapo jana lakini vyombo vya habari vya Ujerumani ikiwemo gazeti la Der Spiegel na kituo cha televisheni cha NTV viliripoti kwamba kansela Olaf Scholz huenda akatoa idhini hiyo hii leo.

Scholz pia anatarajiwa kuidhinisha mataifa mengine  ikiwemo Poland, kupeleka vifaru hivyo vya Leopard nchini Ukraine.

Hata hivyo msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov ameonya kuwa kupelekwa kwa vifaru hivyo nchini Ukraine kutaharibu uhusiano wa siku za usoni kati ya Urusi na Ujerumani. Kwengineko Marekani inataka kutoa ridhaa ya kutumwa kwa vifaru chapa M1 Abrams nchini Ukraine.