1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUjerumani

Ujerumani yakubali kuipatia Ukraine vifaru chapa Leopard 2

Sylvia Mwehozi
25 Januari 2023

Hatimaye Ujerumani imekubali kupeleka vifaru vyake vya kijeshi chapa Leopard 2 ili kuisaidia Ukraine kupambana na uvamizi wa Urusi hatua ambayo imekaribishwa na Kyiv na washirika wake lakini ikilaaniwa vikali na Moscow.

https://p.dw.com/p/4MguH
Deutschland Bundeswehr Kampfpanzer Leopard 2 A7V
Picha: Moritz Frankenberg/dpa/picture-alliance

Kulingana na msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit, Berlin itatoa vifaru 14 chapa ya Leopard 2 A6kutoka kwenye hifadhi yake ya jeshi la Ujerumani Bundeswehr. Uamuzi huo wa Ujerumani unapisha njia kwa nchi nyingine kama vile Poland, Uhispania, Finalnd, Uholanzi na Norway kutuma vifaru chapa ya Leopard kuisaidia Ukraine.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akiwa bungeni leo ametetea uamuzi wa serikali yake akisema kuwa katika kutoa usaidizi wa kijeshi kwa Ukraine, Ujerumani inawajibika kulingana na kanuni ya kile kilicho na umuhimu wakati ikiepuka kuongeza mvutano baina ya Urusi na Jumuiya kujihami NATO. Scholz amekataa shutuma za kwamba Ujerumani imechukua hatua kidogo katika kuisadia Ukraine na misaada ya kijeshi, akisema kwamba "Ujerumani itakuwa mstari wa mbele linapokuja suala la kuisadia Ukraine".

Deutschland | Kampfpanzer Leopard 2
Vifaru chapa Leopard 2 vinavyotengenezwa UjerumaniPicha: Peter Steffen/dpa/picture alliance

"Tutatoa vifaru  vya vita kwa Ukraine, chapa ya Leopard 2. Haya ni matokeo ya mashauriano ya kina na washirika wetu na washirika wa kimataifa. Na ninataka kusisitiza kwamba ilikuwa sawa na ni sawa kwamba hatukuruhusu mtu yeyote kutushinikiza,  lakini badala yake tulitegemea ushirikiano huu wa karibu katika suala hili maalum na tutaendelea kufanya hivyo."

Mara baada ya tangazo hilo, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemshukuru Kansela Scholz kwa uamuzi wa kutuma vifaru hivyo vilivyo na nguvu pamoja na kutoa idhini kwa mataifa mengine kutoa vifaru vyake. Ameandika kupitia ukurasa wa Twitter baada ya kuarifiwa kwa njia ya simu na Kansela Scholz kwamba "shukrani za dhati kwa Kansela na marafiki zetu wote".

Naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekaribisha uamuzi huo wa Berlin. Katika taarifa yake Ikulu ya Elysee imesema kwamba uamuzi huo "unapanua na kuongeza msaada ambao tunautoa wa usambazaji wa AMX10 RC"  akimaanisha gari za kivita zilizotengenezwa Ufaransa ambazo Paris inalenga pia kuipatia Ukraine.

Deutschland Bundeskanzler Scholz spricht vor dem Bundestag
Kansela Olaf Scholz akitetea uamuzi wa kutua vifaru vya Leopard kwa UkrainePicha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki, ambaye aliomba idhini ya Ujerumani kutuma vifaru hivyo, aliishukuru Berlin kwa uamuzi huo na kuuita "hatua kubwa kuelekea kuisimamisha Urusi".

Soma pia: Ujerumani yaashiria kulegeza msimamo kuhusu vifaru vya Leopard kupelekwa Ukraine

Lakini balozi wa Urusi nchini Ujerumani Sergei Nechaev ameonya kwamba "uamuzi huo ni wa hatari sana na unaupeleka mzozo katika kiwango kipya cha makabiliano, na unakinzana na matamshi ya wanasiasa wa Ujerumani kuhusu kutotaka shirikisho la Ujerumani kujihusisha na mgogoro huo". Urusi imeonya hii leo kwamba kama nchi za magharibi zitathubutu kuipatia Ukraine vifaru hivyo basi itaviteketeza katika uwanja wa mapambano.

Msemaji wa Ikulu ya Urusi Kremlin Dmitry Peskov amenukuliwa akisema kwamba "vifaru hivyo vitachomwa kama vingine. Na viko ghali". Tahadhari hiyo ya Kremlin imetolewa wakati kukiwa na taarifa kwamba vikosi vya Urusi vimesonga mbele katika mji wa Bakhmut mashariki mwa Ukraine ambao Urusi imekuwa ikijaribu kuuteka kwa miezi kadhaa.