1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ujerumani: Wanasiasa wakosoa kukwama kupeleka vifaru Ukraine

Zainab Aziz Mhariri: Sylvia Mwehozi
21 Januari 2023

Ujerumani inakabiliwa na upinzani mkali na lawama kutoka kwa nchi washirika kutokana na kusita kwa sasa kuipatia Ukraine vifaru aina ya Leopard ili kuisaidia Ukraine kupambana na Urusi.

https://p.dw.com/p/4MXJO
Litauen Camp Adrian Rohn 2022 | Leopard 2-Panzer der Bundeswehr
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya Baltic wametoa wito kwa Ujerumani kuipa Ukraine vifaru aina ya Leopard baada ya Ujerumani kushindwa kutoa hakikisho la kupeleka vifaru hivyo wakati wa mkutano uliowakutanisha washirika wa Ukraine katika kambi ya kijeshi ya Ramstein kwenye jimbo la Rheinland-Pfalz kusini-magharibi mwa Ujerumani.

Katikati: Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius.
Katikati: Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius. Picha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Ukraine mnamo siku ya Jumamosi ililaumu kitendo cha washirika wake wenye nguvu duniani kushindwa kufikia maamuzi juu ya kuipelekea nchi silaha nzito za kisasa. Mmshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak amesema kwa nchi hizo kushindwa kufikia uamuzi raia wa Ukraine wanazidi kufa.

Soma:Zelensky:Muhimu ni vifaru chapa Leopard

Washirika kadhaa wamemuunga mkono Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa kusema kuwa vifaru hivyo aina ya Leopars ni muhimu kwa Ukraine katika vita dhidi ya jirani yake Urusi.

Mawaziri wa ulinzi wa jumuiya ya kijeshi ya NATO na washirika wa Ukraine walishindwa kufikia uamuzi juu ya usafirishaji wa vifaru hivyo aina ya Leopard-2 kwenye mkutano wao. Hata hivyo waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema nchi yake iko tayari kusonga haraka na hatua hiyo ikiwa makubaliano yatafikiwa.

Kushoto: Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin. Kulia: Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius.
Kushoto: Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin. Kulia: Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius.Picha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Waziri Pistorius amesema Ujerumani kwa sasa haitaki kuchukua hatua ya upande mmoja, na amesisitiza kuwa nchi yake inaweza kupeleka vifaru hivyo nchini Ukraine kwa kushirikiana na washirika wake, ingawa ndani na nje ya nchi miito inaongezeka ya kupeleka nchini Ukraine silaha nzito za kisasa na nzito kuisaidia nchi hiyo.

Soma:Ujerumani: Bado hakuna mwafaka wa kupeleka vifaru Ukraine

Mwanasiasa wa chama cha FDP kilicho kwenye serikali ya muungano amesema Ujerumani imeshindwa kuonyesha uungaji mkono madhubuti kwa Ukraine kwa kuahirisha uamuzi wa kupeleka vifaru vya hali ya juu katika nchi hiyo inayokabiliwa na vita. Marie-Agnes Strack-Zimmermann, mwenyekiti wa kamati ya ulinzi katika bunge la Ujerumani, ametoa maoni hayo baada ya viongozi wa nchi za Magharibi kushindwa kufikia muafaka wa kuipelekea Ukraine vifaru aina ya Leopard-2 vinavyotengenezwa Ujerumani wakati wa mazungumzo mjini Ramstein, Ujerumani.

Mbali na suala hilo Ujerumani na washirika wengine wa nchi za Magharibi waliohudhuria mkutano wa Ramstein wametangaza msaada zaidi kwa Ukraine pamoja na silaha zaidi kwa nchi hiyo.

Kushoto: Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius. Katikati: Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin. Kulia: Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksii Reznikov.
Kushoto: Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius. Katikati: Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin. Kulia: Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksii Reznikov.Picha: Andre Pain/AFP/Getty Images

Washirika hao wa nchi za magharibi siku ya Ijumaa waliyadidimiza matumaini ya Ukraine juu ya kupelekewa kwa haraka vifaru ili kuiongezea Ukaraine nguvu katika vita vyake dhidi ya vikosi vya Urusi kwenye majira yajayo ya joto.

Maafisa wakuu wa Marekani wameishauri Ukraine isimamishe kwanza kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya majeshi ya Urusi hadi itakapopata silaha za kisasa kutoka Marekani pamoja na hatua zamafunzo zitakapokamilika. Hayo ni kwa mujibu wa afisa mmoja mkuu katika utawala wa rais Joe Biden.

Vyanzo: DPA/AFP