Ukraine inataka kuhakikishiwa nafasi Umoja wa Ulaya
12 Mei 2022Akiwa ziarani mjini Berlin, Kuleba Alhamisi amekiambia kituo cha utangazaji cha ARD, kwamba sio kuhusu uwanachama wa haraka kwa Ukraine katika umoja huo, lakini kilicho muhimu sana kwao ni kwamba nafasi hiyo iwe pekee kwa ajili ya Ukraine.
"Mara nyingi tunasikia kwamba Ukraine ni ya Ulaya, ni ya familia ya Ulaya, na sasa ni kuhusu kuhakikisha tunahifadhi sehemu hiyo," alisisitiza Kuleba.
Mapema wiki hii, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alionya kwamba itachukua miongo kadhaa kwa nchi inayotaka kujiunga kama vile Ukraine kuingia katika Umoja wa Ulaya.
Kuleba, ambaye yuko mjini Berlin kukutana na viongozi wa kisiasa wa Ujerumani na pia kuhudhuria mkutano na mawaziri wenzake wa kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7, amesema atajadili kuhusu vikwazo zaidi kwa Urusi kutokana na uvamizi wake Ukraine.
Ama kwa upande mwingine, taarifa za kijasusi za jeshi la Uingereza zimeeleza kuwa vikosi vya Ukraine vimefanikiwa kuchukua tena udhibiti katika miji na vijiji kadhaa kuelekea kwenye mpaka wa Urusi kaskazini mwa mji wa Kharkiv.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Uingereza, vikosi vya Ukraine vimefanikiwa kusonga mbele baada ya Urusi kuondoa vikosi vyake kutokana na kushambuliwa.
Maafisa wa jeshi la Ukraine wamesema kwa sasa vikosi vya Urusi vimeongeza mashambulizi makali kuelekea jimbo lake la mashariki la Donbas. Ukraine imesema adui yake huyo analenga kuchukua udhibiti kamili wa Donetsk, Luhansk na Kherson.
Watu watatu wauawa kwenye shambulizi la Urusi
Aidha, taarifa za idara za dharura zinaeleza kuwa watu watatu waliuawa na wengine 12 walijeruhiwa Jumatano katika shambulizi la Urusi kaskazini mashariki mwa Ukraine, katika mji wa Chernigiv ulioko umbali wa kilomita 45 kusini mwa mpaka wa Urusi.
Wakati huo huo, Rais wa Finland Sauli Niinisto amesema anaunga mkono nchi hiyo kuomba uwanachama wa Jumuia ya Kujihami ya NATO. Hatua hiyo itafungua njia ya kutanuka kwa jumuia hiyo baada ya Urusi kuongeza vitisho vyake.
Huku hayo yakijiri, mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine, Iryna Venediktova amesema ofisi yake imemfungulia mashtaka afisa wa jeshi la Urusi kwa kuhusika na mauaji ya raia aliyepigwa risasi wakati akiendesha baiskeli.
Afisa huyo mwenye cheo cha Sajenti mwenye umri wa miaka 21, alimuua mzee huyo katika kijiji cha Chupakhivka. Venediktova amesema ofisi yake inachunguza zaidi ya visa 10,700 vya uhalifu wa kivita, huku zaidi ya washukiwa 600 wakiwa wametambuliwa hadi sasa.
Naye mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema leo kuwa mauaji yaliyofanyika kwenye eneo karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kiev katika wiki za hivi karibuni yanaweza kuwa uhalifu wa kivita.
Baraza la Haki za Binaadamu Alhamisi litaamua iwapo liwape wapelelezi kazi ya kuchunguza rasmi matukio yaliyotokea Kiev na miji mingine katika miezi ya Februari na Machi.
(AFP, AP, Reuters, DW)