1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaanzisha mashambulizi kuyakomboa maeneo ya kusini

29 Agosti 2022

Ukraine imetangaza kuwa imeanzisha mashambulizi yaliyosubiriwa kwa muda mrefu kwa lengo la kuyanyakua tena maeneo ya kusini mwa nchi hiyo ambayo yanadhibitiwa na vikosi vya Urusi.

https://p.dw.com/p/4GBgN
DW Still | Krieg in der Ukraine - Soldat im Schützengraben
Picha: DW

Msemaji wa kamandi ya jeshi la kusini mwa Ukraine, Natalia Humeniuk amesema leo kuwa mashambulizi hayo yanafanywa kuelekea maeneo tofauti ikiwemo jimbo la Kherson. Ukraine imekuwa ikizungumzia juu ya mpango wa kukabiliana na mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na Urusi kusini mwa nchi hiyo kwa muda wa miezi miwili. Operesheni hiyo inayoonesha imani ya Ukraine ikiongezeka wakati ambapo msaada wa kijeshi wa nchi za Magharibi ukiendelea kuingia nchini humo.

Mashambulizi yaidhoofisha Urusi

Humeniuk amesema kwamba mashambulizi ya hivi karibuni ya Ukraine kwenye njia za kimkakati za kusini mwa Urusi zimemdhoofisha adui yao na kuongeza kuwa zaidi ya maghala 10 yenye silaha za kijeshi za Urusi yameshambuliwa wiki iliyopita. Hata hivyo, hakufafanua zaidi kuhusu mashambulizi mapya, akisema operesheni yoyote ya kijeshi inahitaji utulivu.

Aidha, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Urusi, Igor Konashenkov amesema makombora ya Ukraine yanashambulia karibu na kinu cha nyuklia. ''Mashambulizi ya vikosi vya Ukraine katika mji wa Energodar uliopo karibu na kinu cha nyuklia hayasimami. Kwa siku moja iliyopita, makombora nane ya Ukraine yamefyatuliwa katika maeneo ya makaazi kwenye mji. Raia ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa. Makombora mawili yameripuka karibu na eneo la kinu cha nyuklia,'' alifafanua Konashenkov.

Ukraine Kiew | Pressekonferenz: Wolodymyr Selenskyj
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: Ruslan Kaniuka/Ukrinform/ABACA/picture alliance

Wakati huo huo, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameishutumu Urusi kwa ugaidi wa kiuchumi kwa kujaribu kuyazuia mataifa ya Ulaya kuhifadhi gesi kabla ya msimu wa baridi wakati ambapo athari ya kupanda kwa ankara za nishati zitakapozikumba vibaya kaya na biashara. Zelensky ameyatoa matamshi hayo Jumatatu kwa njia ya video katika mkutano wa nishati unaofanyika Norway.

Kauli yake inajiri wakati ambapo kampuni ya gesi ya Urusi, Gazprom inapanga wiki hii kufanya matengenezo ya kusitisha usambazaji wa gesi kupitia bomba la gesi unaojulikana kama Nord Stream 1 linaloziunganisha Urusi na Ujerumani kupitia Bahari ya Baltic. Hatua hiyo imezidisha hofu kwamba Urusi inazuia usambazaji ili kuweka shinikizo kwa mataifa ya Magharibi yanayopinga uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, madai ambayo nchi hiyo imeyakanusha.

G7 yapongeza ujumbe wa IAEA kuzuru Zaporizhizhia

Ama kwa upande mwingine, kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7, limepongeza hatua ya wataalamu wa Shirika la Kimataifa la kudhibiti matumizi ya Nishati ya Nyuklia, IAEA, kukitembelea kinu cha nyuklia cha Zaporizhizhia kilichoko nchini Ukraine. Nchi hizo zimesema katika taarifa yake kwamba pamekuwa na wasiwasi mkubwa na kitisho kinachowekwa na vikosi vya Urusi kutokana na kuendelea kudhibiti maeneo ya kinu hicho.

Huku hayo yakijiri, Uholanzi imesema itapeleka timu tatu zaidi za wachunguzi nchini Ukraine kwa ajili ya kusaidia uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC kuhusu uhalifu wa kivita tangu Urusi ilipoivamia Ukraine. Hatua ya kupelekwa kwa wachunguzi hao mwishoni mwa mwaka huu na mwaka ujao, inafuatiwa na kupelekwa kwa wapelelezi kadhaa wa Uholanzi nchini Ukraine mwezi Mei, kama sehemu ya ujumbe mkubwa wa ICC kupelekwa katika historia ya mahakama hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Wopke Hoekstra amesema bado wana nia ya kujitolea kikamilifu kwa ajili ya haki kutokana na uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

(DPA, AFP, Reuters)