Ukraine yawaamuru wanajeshi wa Azovstal kuweka chini silaha
20 Mei 2022Kamanda wa kikosi cha walinzi wa taifa cha Azov, Denys Prokopenko, amesema uongozi wa juu wa jeshi umetoa agizo hilo ili kuyanusuru maisha na afya za wapiganaji hao na kuacha kuulinda mji huo. Akizungumza Ijumaa katika ujumbe alioutoa kwa njia ya video, Prokopenko amesema mchakato wa kuwaondoa wanajeshi waliouawa unaendelea.
"Licha ya mapigano makali na ukosefu wa vifaa, tumesisitiza mara kwa mara masharti matatu muhimu zaidi kwetu, hasa kuwaondoa raia, waliojeruhiwa na waliouawa. Raia walihamishwa. Waliojeruhiwa vibaya wamepewa msaada muhimu unaohitajika na tumefanikiwa kuwaondoa na tumewahamishiwa kwenye eneo linalodhibitiwa na Ukraine," alisisitiza Prokopenko.
Kwa mujibu wa duru za Urusi, zaidi ya wanajeshi 1,900 wa Ukraine wamejisalimisha kutoka kwenye kiwanda cha Azovstal, na tayari wamechukuliwa kama wafungwa. Hata hivyo, inasemekana kuwa makanda wa kikosi hicho wamebakia kwenye mahandaki katika kiwanda cha Azovstal.
Wakati huo huo, mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu wa kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7, wamesema wamekusanya takribani dola bilioni 20 kwa ajili ya Ukraine na wameahidi kutoa msaada zaidi wa kifedha iwapo itahitajika.
Taarifa iliyotolewa Ijumaa kufuatia mkutano wa mawaziri hao nchini Ujerumani, imeeleza kuwa mwaka 2022, wameahidi dola bilioni 19.8 ya bajeti ya msaada, ikiwemo dola bilioni 9.5 ya ahadi ya hivi karibuni kuisaidia Ukraine kuziba pengo lake la kifedha na kuendelea kuhakikisha utoaji wa huduma muhimu na za msingi kwa watu wa Ukraine.
Schroeder ajiondoa kwenye kampuni ya Rosnet
Huku hayo yakijiri, kansela wa zamani wa Ujerumani, Gerhard Schroeder ameiambia kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya Urusi ya Rosnet kwamba hawezi kuendelea kuwepo katika bodi yake ya wakurugenzi.
Taarifa hizo zimechapishwa Ijumaa katika tovuti ya kampuni ya Rosnet. Tovuti hiyo pia imesema mfanyabiashara wa Ujerumani, Matthias Warning pia amechukua hatua kama hiyo.
Rosnet imesema wanaunga mkono uamuzi wao na wanawashukuru kwa kuendelea kuwaunga mkono. Schroeder amekuwa akikosolewa vikali kwa kuendelea na wadhifa huo, licha ya Urusi kuivamia Ukraine.
Ama kwa upande mwingine, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema anazungumza na viongozi wa mataifa ya Magharibi kuhusu msimamo wa nchi yake wa kupinga kuzikaribisha Sweden na Finland kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Aidha, Ujerumani imesema itaipatia Ukraine makombora 15 ya kujilinda dhidi ya vifaru mwezi Julai. Wizara ya Ulinzi ya Ujerumani imesema Ijumaa kuwa mbali na msaada wa silaha, pia vikosi vya Ujerumani vitatoa mafunzo na msaada wa risasi 60,000. Tangazo hilo limetolewa baada ya mkutano uliofanyika Ijumaa kati ya Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Christine Lambrecht na waziri mwenzake wa Ukraine, Olexii Resnikov.
(AFP, DPA, Reuters, DW)