1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaendeleza mashambulizi Ukraine

20 Mei 2022

Rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky amesema hatua ya Urusi kuanzisha tena mashambulizi kwenye jimbo la Donbas imeuharibu kabisa mkoa huo wa mashariki mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Bcf1
Ukraine-Krieg | Gefechte im Donbass
Picha: Alex Chan Tsz Yuk/SOPA Images/ZUMA Press/picture alliance

Akizungumza usiku wa kuamkia Ijumaa, Zelensky amesema ingawa vikosi vya jeshi la Ukraine vinasonga mbele kuukomboa mkoa wa Kharkiv, vikosi vya Urusi vinajaribu kuongeza shinikizo na vinataka kuchukua udhibiti kamili wa Donbas, eneo ambako wananchi wake wanazungumza Kirusi, ambalo tangu mwaka 2014 limekuwa likidhibitiwa na waasi wanaotaka kujitenga ambao wanaiunga mkono Urusi.

"Vikosi vya Urusi vimeufanya mji wa Donbas kuharibika vibaya. Huo ni ukweli. Mashambulizi katika mji wa Severodonetsk ni ya kikatili na haana maana. Watu 12 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika kipindi cha siku moja tu," alifafanua Zelensky.

Severodonetsk imelengwa kwa muda mrefu

Mkoa wa Severodonetsk umekuwa ukilengwa na mshambulizi ya mabomu ya Urusi katika siku za hivi karibuni. Magavana wa mikoa ya Kharkiv na Donetsk wamesema kuwa watu sita wamekufa katika mikoa hiyo.

Kwa mujibu wa Zelensky, Urusi ina nia ya kuwaua wananchi wengi wa Ukraine iwezekenavyo na kufanya uharibifu mkubwa kwenye nchi hiyo. Ameongeza kusema kuwa hiyo ni siasa na sera ya mauaji ya kimbari.

Ukraine-Krieg Mariupol | Abtransport von Kriegsgefangenen aus Asow-Stahlwerk
Basi lenye wanajeshi wa Ukraine walioondolewa kwenye kiwanda cha AzovstalPicha: AP Photo/picture alliance

Huku hayo yakijiri Urusi imesema idadi ya wanajeshi wa Ukraine waliojisalimisha katika kiwanda cha chuma cha Azovstal, kwenye mji wa Mariupol imefikia 1,730.

Ukraine iliwashawishi wanajeshi hao kuondoka kwenye kiwanda hicho ili kuyaokoa maisha yao, baada ya kukaa kwenye eneo hilo la kiwanda kwa wiki kadhaa bila ya kuwa na chakula, maji na dawa.

Scholz: Kujiunga Umoja wa Ulaya ni mchakato mrefu

Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema hakuna njia ya mkato kwa Ukraine kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Amesema kuipendelea Ukraine, haitokuwa haki kwa mataifa mengine ya Balkan Magharibi ambayo yameomba pia kujiunga na umoja huo. Scholz amesema mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya ni wa muda mrefu.

Naye Balozi wa Ukraine nchini Ujerumani, Andrij Melnyk ametilia shaka dhamira ya Scholz kutaka kuipatia silaha Ukraine. Akizungumza Ijumaa na shirika la habari la RND lenye makao yake mjini Hanover, Melnyk amesema wanahisi kwamba kansela huyo wa Ujerumani hataki kutoa silaha hizo.

Bilderchronik des Krieges in der Ukraine | Berlin | Ukrainischer Botschafter Melnyk bei Eröffnung der Foto-Ausstellung „Ukraine
Balozi wa Ukraine nchini Ujerumani, Andrij MelnykPicha: Jörg Carstensen/dpa/picture alliance

Nalo Bunge la Marekani, limeidhinisha msaada mwingine wa dola bilioni 40 kwa ajili ya Ukraine. Ikulu ya Marekani imesema Rais Joe Biden atasaini msaada huo akiwa katika ziara yake barani Asia.

Ama kwa upande mwingine, wakili wa mwanajeshi wa kwanza wa Urusi anayeshtakiwa kwa uhalifu wa kivita mjini Kiev, amesema Ijumaa kuwa mteja wake hana hatia ya mauaji ya kukusudia na uhalifu wa kivita, ingawa amekiri kumuua raia.

Wakili huyo, Viktor Ovsyannikov ameiomba mahakama imuachilie huru mteja wake. Mshatakiwa huyo leo ameomba radhi na kusema anasikitishwa sana na kitendo alichokifanya.

Nao mawaziri wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya wanakutana Ijuma kujadiliana kuhusu madhara yanayosababishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mmoja wa wakulima wakubwa wa nafaka duniani.

(AFP, DPA, Reuters, DW)