Ulaya yaiomba Iran kuharakisha mazungumzo ya nyuklia
18 Desemba 2021Ujumbe wa Ulaya kwenye mazungumzo ya kuufufua mkataba wa nyuklia wa Iran wameliomba taifa hilo kufanya haraka kuuokoa mkataba huo baada ya kuanza kwa raundi ya saba ya mazungumzo mjini Vienna.
Wawakilishi hao wa Ulaya kutoka Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wanaotambulika kama E3 wameiita hatua ya mapumziko ya siku chache ya mazungumzo hayo kuwa ni ya kukatisha tamaa, ingawa wanakiri kuwepo na maendeleo ya kiufundi.
Mmoja wa wajumbe hao Enrique Mora ameviambia vyombo vya habari kwamba kuna umuhimu wa kuwepo na udharura ikiwa kweli wanataka kuwa na mafanikio katika mazungumzo hayo. Amesema "hatuna miezi, ni afadhali tukawa na wiki chache ili kufikia makubaliano".
Bado haijulikani ni kwa nini maafisa wa Iran waliomba mapumziko ya mazungumzo hayo.
Soma Zaidi: Marekani, Israel waijadili Iran ikigoma kurudi kwenye makubaliano ya nyuklia
"Ikiwa upande mwingine utakubaliana na sababu zenye mantiki za Iran, duru inayofuata ya mazungumzo inaweza kuwa ya mwisho," alisema mpatanishi mkuu wa Iran Ali Bagheri Kani.
Raundi hii ya mazungumzo imeanza Novemba 29, ikiwa ni mara ya kwanza tangu rais mwenye msimamo mkali wa Iran Ebrahim Raisi alipoingia madarakani mwezi Agosti.
IAEA imekuwa ikionya Iran inaongeza urutubishaji wa urani.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya nyuklia limeonya kuwa Iran inarutubisha madini ya urani, kinyume na makubaliano haoy ya mwaka 2015.
Wapatanishi kutoka serikali ya Marekani pia wameshiriki kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika duru hii ya sasa ya majadiliano. Biden alisema hapo awali kuwa hataondoa vikwazo dhidi ya Iran hadi pale Tehran itakapositisha shughuli zake za kurutubisha urani.
Soma Zaidi: IAEA: Iran inaongeza akiba yake ya madini ya urani
Ingawa maafisa wa Biden wanaamini kuwa makubaliano ya kidiplomasia ndio njia bora zaidi ya kuwasiliana na Iran, gazeti la New York Times liliripoti wiki iliyopita kwamba Ikulu ya White House ilikuwa inapitia machaguo ya kijeshi kwa lengo la kuizuia Tehran kupata silaha za nyuklia.
Marekani ilijiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya Iran, ya JCPOA chini ya rais wa zamani Donald Trump, ambaye aliamini kuwa makubaliano hayo hayakuwa na tija. Mataifa yaliyosalia kwenye makubaliano hayo yalikuwa ni Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Urusi, China na Umoja wa Ulaya.
Soma Zaidi: Iran kuanza tena mazungumzo ya nyuklia
Mashirika: DW