1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu wahimiza kuyathamini Maji

22 Machi 2021

Umoja wa Mataifa umetowa mwito wa kuchukuliwa hatua ya uwekezaji mkubwa katika upatikanaji wa rasilimali muhimu ya maji duniani. kutokana na ripoti ya UN kuhusu maendeleo yanayotokana na maji duniani ya mwaka 2021.

https://p.dw.com/p/3qy5n
Weltspiegel 05.03.2021 | Simbabwe Bulawayo | Zugang Trinkwasser
Picha: KB Mpofu/Getty Images

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imechapishwa leo Jumatatu na miongoni mwa mambo yaliyosisitizwa ni kutambuliwa umuhimu wa bidhaa hiyo.

Ripoti hiyo imeweka kipimo na kuzungumzia wazi umuhimu wa maji duniani pamoja na kuonesha umuhimu wa kushirikishwa suala la maji katika utolewaji maamuzi kama hatua ya msingi kabisa ya kufikia maendeleo endelevu na usimamizi thabiti wa rasilimali ya maji sambamba na maendeleo endelevu yaliyowekwa katika malengo ya Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo iliyokusanywa na kuchapishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO inaeleza kwamba mara nyingi thamani ya maji haipewi umuhimu katika michakato ya utowaji maamuzi.

soma zaidi: Uhaba wa maji waitatiza dunia

Ripoti hiyo imekwenda mbali zaidi na kueleza kwamba kimsingi thamani ya bidhaa hiyo katika jamii imemezwa na miundombinu inayojengwa kwa ajili ya kuyahifadhi au kuyasafirisha maji hayo kwa maneno mengine miundo mbinu inaonekana kuwa ya faida zaidi kuliko raslimali hiyo ya maji.

Ripoti hiyo pia inaeleza kwamba hata hivyo baadhi ya miradi ya miundo mbinu  inaonesha kuwepo kwake kunategemea hayo hayo maji na mwishowe miradi hiyo haina maana. Kufujwa na kuchafuliwa kwa maji ni miongoni mwa changamoto nyingine kwa mujibu wa Umoja huo wa mataifa.

Ukosefu wa huduma ya maji yatatiza juhudi za kukabiliana na Virusi vya corona 

USA Migranten Grenze Mexiko Texas USA
Picha: DANIEL BECERRIL/REUTERS

Janga la virusi vya corona limeongeza matatizo makubwa kwa watu wanaoishi kwenye mitaa ya madondo poromoka na makaazi yasiyokuwa rasmi. Imetajwa kwamba duniani kote,zaidi ya watu bilioni 3 hawana huduma ya maji na vituo viwili kati ya kila vitano  vinakosa huduma ya maji ya kunawa mikono, huduma muhimu zaidi katika hatua ya kuzuia kuenea magonjwa kama Covid-19.

Jana kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis naye pia alizungumzia suala hilo la umuhimu wa maji duniani akisema ulimwengu unapaswa kuhakikisha kila mmoja anapata huduma hiyo.

soma zaidi: Siku ya Maji duniani - hali visiwani Zanzibar

Nchini Nigeria kwa mfano kiasi thuluthi moja ya watoto nchini humo hawana huduma ya kupata maji ya kutoka kwa mujibu wa shirika linalohusika na masuala ya watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF ambalo limetowa mwito hatua za haraka zichukuliwe kulishughulikia tatizo hilo.

Watu bilioni 1.42 wakiwemo watoto milioni 450 wanaishi maeneo yenye ukosefu mkubwa wa maji duniani kwa mujibu wa Unicef.Kiasi watoto laki moja Nigeria wanatajwa kufa kila mwaka kutokana na magonjwa yanayosiana na maji.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu maji imetowa mwito wa kutafutwa njia mpya za kuangalia umuhimu wa maji  na mwelekeo wa kushughulikia suala hilo kwa kutambua kwamba maji ni uhai na hayana mbadala.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW