UN yabaini dalili za uhalifu wa kivita Ukanda wa Gaza
2 Januari 2024Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja Mataifa Volker Türk amesema kuna dalili za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu kwenye Ukanda wa Gaza.
Kamishna Türk ametoa mfano wa shambulio la nchini Israeli la Oktoba 7 pamoja na mashambulio ya kiholela dhidi ya Israel na hatua za kijeshi kwenye sehemu za raia.
Kuhusu hatua za Israeli, Türk ameliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA, mjini Geneva kwamba ana wasiwasi mkubwa iwapo nchi hiyo inazingatia haki za binadamu na sheria za kimataifa katika hatua inazochukua.
Soma taarifa inayohusiana na hii: UN: Hatari ya uhalifu wa kivita ni kubwa Gaza
Kamishna huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa asilimia 70 ya wale walioathirika na mashambulizi makubwa ya Israel ni wanawake na watoto. Türk, amesema kuwaadhibu Wapalestina wote kwa pamoja ni uhalifu wa kivita na kwamba uchunguzi wa kina unahitajika.