Umoja wa Mataifa waituhumu RSF kwa uhalifu wa kivita Darfur
1 Machi 2024Wataalamu hao walisema vikosi vya RSF pamoja na wanamgambo washirika wake wanaopigana kuchukuwa madaraka nchini Sudan walifanya mauaji ya kikabila na kuwabaka wanawake, huku wakichukuwa udhibiti wa maeneo makubwa ya magharibi mwa jimbo la Darfur.
Soma zaidi: Pande hasimu zatenda uhalifu wa kivita Sudan - UN
Kulingana na ripoti mpya ya wataalamu hao, matukio hayo yanaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Ripoti hiyo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo shirika la habari la Associated Press limepata nakala yake, ilionesha taswira ya kutisha ya ukatili wa wanamgambo hao, ambao wengi wana asili ya Kiarabu dhidi ya Waafrika wa Darfur.
Sudan ilitumbukia kwenye machafuko mnamo mwezi Aprili kufuatia uhasama wa muda mrefu kati ya jeshi la taifa linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na kikosi cha RSF kinachoongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo.