Umoja wa Mataifa kupambana na ubakaji wakati wa vita
24 Aprili 2019Baraza la Usalama lililazimika kukubali masharti ya Marekani hapo jana, iliyosema lugha iliyotumika kuelezea kipengele kinachohusiana na haki ya mwanamke juu ya suala la afya ya uzazi isitumiwe katika azimio hilo lenye lengo la kupambana na unyanyasaji wa kijinsia unaowakumba wanawake katika maeneo ya vita.
Marekani ilitishia kulipinga azimio hilo lilowasilishwa na Ujerumani kwa kutumia kura yake ya turufu iwapo hakitondolewa kipengele kinachotaja umuhimu wa kutoa msaada wa haraka kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsa na kuwapa haki ya kutoa mimba.
Marekani imedai kwamba maelezo hayo yanachochea utoaji wa mimba. Azimio hilo hatimaye lilipitishwa baada ya kipengele kizima kilichokataliwa na Marekani kufutwa.
Delattre: "waanawake wana haki ya kutoa mimba"
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas ameitaja kuwa ni hatua muhimu. Lakini balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Francois Delattre ameliambia Baraza la Usalama baada ya kupiga kura kwamba ni kitu kisichoeleweka kwa baraza hilo kushindwa kutambua kuwa wanawake na wasichana waliokabiliana na unyanyasaji wa kijinsia katika vita - na ambao bila shaka hawakutaka kushika mimba- lazima wapewe haki ya kuzitoa mimba hizo.
Akiwa katika mkutano huo wa Baraza la Usalama, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameliunga mkono azimio hilo.
"Tunapaswa kutambua kwamba unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo yenye migogoro unawathiri zaidi wanawake na wasichana kwa sababu unahusishwa kwa karibu na masuala ya ukosefu wa usawa wa kijinsia pamoja na ubaguzi. Ili kuzuia hali hiyo lazima tuzingatie kuendeleza haki za wanawake na usawa wa kijinsia wakati wote, kabla, wakati na baada ya migogoro," amesema Antonio Guterres.
China na Urusi pia zilipinga lugha iliyotumika katika azimio hilo, lakini hazikutishia kutumia kura ya turufu badala yake hazikupiga kura kabisa.
Azimio hilo limepitishwa katika wakati ambapo Ujerumani inashika hatamu ya urais ya mwezi mmoja katika baraza hilo.
Washindi wa tuzo ya Nobeli Nadia Murad na Denis Mukwege, pamoja na mwanasheria wa Haki za Binadamu Amal Clooney, pia walihudhuria na kuchangia katika majadiliano hayo ya siku nzima kuhusu unyanyasaji wa kijinsia wa wanawake katika maeneo yenye vita.