1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSyria

Umoja wa Mataifa watoa wito wa kuwasaidia waathirika, Syria

15 Februari 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kupatikana msaada wa kibinaadamu wa dola milioni 397 kwa ajili ya watu milioni 5 katika eneo linaloshikiliwa na waasi kaskazini magharibi mwa Syria.

https://p.dw.com/p/4NWAt
UN-Generalsekretär Antonio Guterres
Picha: Selcuk Acar/AA/picture alliance

Watu hao milioni tano ni ambao wameathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi la wiki iliyopita lililozipiga Syria na Uturuki huku vifo kufuatia janga hilo vikikaribia 40,000.

Guterres ametoa wito huo hapo jana ili kuwasaidia watu hao ambao hadi sasa wamepata usaidizi mdogo kutokana na  mgawanyiko mkubwa uliosababishwa na vita vya miaka 12 nchini  Syria.

UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Antonio Guterres, UN-Generalsekretär
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Andrej Ivanov/AFP/Getty Images

Katibu Mkuu huyo ametoa pia wito huo siku moja baada ya kupongeza makubaliano kati ya Umoja wa Mataifa na Rais wa Syria Bashar al Assad, ya kufungua vivuko vingine viwili kutokea Uturuki na kwa kipindi cha miezi mitatu ili kufanikisha usafirishaji wa misaada hiyo.

Hadi sasa Umoja wa Mataifa umeruhusiwa tu kupeleka msaada katika eneo la kaskazini-magharibi la Idlib kupitia kivuko kimoja cha Bab Al-Hawa. Guterres amesema wamo katika hatua za mwisho ili kutoa wito kama huo kwa ajili ya Uturuki.

Soma pia:Umoja wa Mataifa: Shughuli za uokozi zinakaribia kumalizika Uturuki, Syria 

Syrien | Landwirtschaft | Dürre 2010
Wakulima wa Syria wakiwa katika mashamba huko Daraa, Kilometa 100 kutoka mji mkuu Damascus.Picha: Louai Beshara/AFP/Getty Images

Guterres ameitaka jumuiya ya kimataifa kutoa msaada huo bila kuchelewa, na kusema kuwa mateso ya binadamu kutokana na janga hili la asili hayapaswi kuzidishwa na vizuizi vitokanavyo na binaadamu. Amesisitiza kuwa, upatikanaji, ufadhili, vifaa na misaada lazima vitoke pande zote na kuelekea sehemu zote bila kuwepo vikwazo.

Afisa mkuu wa Shirika la Chakula Duniani katika eneo la Mashariki ya Kati Corine Fleischer ameonya juu ya hali mbaya ya usalama wa chakula katika maeneo yaliyoathirika ya Syria na kusema hali hiyo imekuwa ikiongezeka kwa kasi hata kabla ya tetemeko la ardhi.

Hali nchini Uturuki:

Erdbeben in der Türkei - Kahramanmaras
Jengo lililoporomoka huko Kahramanmaras, kusini mashariki mwa UturukiPicha: Bulent Kilic/AFP

Wizara ya Mipango Miji imesema katika ripoti kuwa jumla ya majengo 50,576 aidha yameporomoka au kuharibiwa vibaya na matetemeko ya ardhi, na majengo hayo yanahitaji kubomolewa haraka.

Mamlaka hadi sasa zimekagua zaidi ya majengo 387,000 katika mikoa 10 ya kusini-mashariki iliyokumbwa na tetemeko la ardhi, huku mji wa Gaziantep ukiwa na idadi kubwa zaidi ya majengo yanayohitaji kubomolewa haraka.

Soma pia: UN:Watoto milioni 7 wameathirika kote Uturuki na Syria

Tetemeko hilo limefufua mahusiano ya kidiplomasia ambapo Waziri wa Mambo   ya Nje wa Armenia Ararat Mirzoyan amefanya ziara adimu kwa hasimu wake Uturuki na kusisitiza nia ya "kujenga amani" baada ya janga la tetemeko la ardhi kusababisha vifo vya karibu watu 40,000.

Tetemeko hilo la juma lililopita limefuatiwa kuanza tena kwa mazungumzo kati ya Uturuki  na wapinzani wake wa kihistoria, wakiwemo Armenia na Ugiriki. Waziri wa mambo ya nje wa Ugiriki alifanya ziara katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko mwishoni mwa juma lililopita, huku mwanadiplomasia mkuu wa Armenia akiwasili mjini Ankara leo Jumatano.