1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya haulitambui kundi la Taliban

21 Agosti 2021

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema umoja huo haulitambui kundi la Taliban na wala hautoshiriki mazungumzo ya kisiasa na kundi hilo.

https://p.dw.com/p/3zKHl
Spanien | Ursula Von der Leyen besucht ein Aufnahmelager evakuierte aus Afghanistan
Picha: Paul White/AP/dpa//picture alliance

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema umoja huo haulitambui kundi la Taliban na wala hautoshiriki mazungumzo ya kisiasa na kundi hilo. Matamshi ya Von der Leyen yamekuja wiki moja baada ya Taliban kuidhibiti Afghanistan ukiwemo mji mkuu Kabul.

Ursula von der Leyen amedokeza hilo akiwa pamoja na rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel, walipokitembelea, kituo kimoja cha wafanyakazi wa Umoja wa Ulaya ambao ni raia wa Afghanistan waliohamishiwa mjini Madrid kutoka Kabul.

Aidha amesema atapendekeza ongezeko la fedha euro milioni 57 zilizohitajika kufanikisha misaada ya kiutu kufikishwa Afghanistan katika kitita cha msaada kilichokuwa tayari kimepitishwa na EU. Amesema msaada wa maendeleo unakwenda sambamba na kuheshimiwa kwa haki za binaadamu, kuwashughulikia vyema watoto walio chini ya miaka 18 na kuheshimu haki za wanawake na wasichana.

Rais huyo wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya amesema wako tayari kutoa msaada kwa Mataifa ya Ulaya ili kuwasaidia wakimbizi na pia amepanga kuwasilisha suala la makaazi kwa wakimbizi hao katika mkutano wa G7 wiki ijayo.

Ujerumani yaahidi kuwaondoa raia wake waliokwama Afghanistan

Annegret Kramp-Karrenbauer zu Anschlag in Mali
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer Picha: Henning Kaiser/dpa/picture alliance

Huku hayo yakiarifiwa Ujerumani imesema itafanya kila iwezalo kuwaondoa raia wake Afghanistan, licha ya operesheni ya kuwarejesha nyumbani kukumbwa na changamoto baada ya vurugu kutokea katika uwanja wa ndege wa Kabul.

Akizungumza mjini Berlin, Waziri wa Ulinzi Annegret Kramp-Karrenbauer amesema hali sio nzuri kwa sasa lakini watatumia kila njia kuhakikisha wanawaondoa raia wote wa Ujerumani nchini Afganistan.

soma zaidi: Biden: Tutawaondoa raia wote Afghanistan

Kwa sasa helikopta mbili za jeshi la Ujerumani zimewasili mjini Kabul leo Jumamosi kusaidia katika mipango ya kuwahamisha raia.

Kwa upande wake Waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz -anaewania kuwa kansela mpya wa Ujerumani baada ya Merkel kumaliza muda wake, amesema katika mahijiano na kituo cha redio cha Deutschlandfunk kwamba Ujerumani itaendelea kuwa tayari kutoa msaada kwa waandishi habari, wafanyakazi wa kiutu na wale walio katika siasa Afghanistan.

Kudorora kwa serikali ya Afghanistan kulianza wakati rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, alipokubali kuwaondoa wanajeshi wa Marekani nchini humo mpango ulioanza kutekelezwa miezi kadhaa mapema kuliko ilivyopangwa na rais wa sasa Joe Biden.

UNHCR yaitaka Ulaya iwasaidie wakimbizi wa Afghanistan

Schweiz Filippo Grandi Flüchtlingskommissar UN
Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Wakati huo huo Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi ameyatolea wito mataifa ya Ulaya kuwasaidia wakimbizi wa Afghanistan ili kuepuka mzozo mkubwa wa wahamiaji kwenye kanda hiyo.

Grandi ameliambia  gazeti moja ya kila siku la nchini Italia kwamba siyo rahisi kwa Ulaya kushuhudia wimbi la wakimbizi wa Afghanistan lakini hilo linategemea aina ya msaada utakaotolewa na kanda hiyo kwa wale watakaoikimbia Afghanistan kwenda mataifa jirani.

soma zaidi: Taliban yawasaka maadui nyumba kwa nyumba

Mkuu huyo wa UNHCR amesema mataifa yatakayoandamwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa Afghanistan ni pamoja na Pakistan, Iran na Tajikistan na Ulaya itapaswa kuwasaidia huko waliko kabla hawajafanya safari kukimbia mazingira magumu.

Chanzo: reuters,dpa