UN: Yaelezea wasiwasi wa mashambulizi ya kigaidi mashuleni
16 Januari 2020Tume ya kuwaajiri walimu nchini Kenya, TSC imeanza shughuli ya kuwahamisha walimu hadi maeneo yaliyo salama katika kaunti ya Wajir.
Uhamisho huo unafanyika katika kaunti hiyo. Haya yanajiri baada ya shambulio la siku chache lililopita kuwaua walimu watatu eneo la Garissa.Waziri wa Elimu Profesa George Magoha anausisitizia umuhimu wa walimu kusalia kwenye kaunti husika.
Walimu wanahofia usalama wao kwasababu ya mashambulio ya kundi la kigaidi la Al Shabaab ambayo yameanza kurejea katika eneo la kaskazini mwa Kenya.
Mwanzoni mwa wiki hii wanamgambo waliojihami kwa silaha nzitonzito walilivamia alfajiri eneo la Kamuthe katika kaunti ya Garissa na kuwaua walimu wa kiume.Waliosalimika ni walimu watatu wa kike na mhudumu mmoja.
Wiki moja iliyopita wapiganaji wanaoaminika kuwa wa kundi hilohilo la Al Shabaab waliivamia shule ya msingi ya Saretho na kuwaua wanafunzi 4 na wengine 3 pamoja na mlinzi kujeruhiwa.
Visa hivyo viwili vimewatia hofu waalimu wanaofanya kazi kwenye kaunti za Garissa, Mandera na Wajir ambao kwa sasa baadhi yao wanataka wahamishiwe kwengine.
Walimu wanaohudumu katika maeneo hatari tayari wameshapewa nyara za kuhamishwa
Kulingana na mkurugenzi wa tume ya kuwaajiri walimu katika kaunti ya Wajir, Solomon Leseewa, walimu wanaohudumu kwenye maeneo yanayopakana katika mpaka wa Kenya na Somalia tayari wameshapewa nyaraka za kuwahamishia hadi shule zinazoaminika kuwa salama zaidi.Walimu hao wameamrishwa kufika kwenye afisi za muajiri wao TSC mjini Wajir kwa maelezo zaidi.
Hata hivyo idadi kamili ya walimu watakaohamishwa haijakuwa bayana.Shule zilizoko maeneo ya Tarbaj na sehemu za Wajir Mashariki na Kusini huenda zikakumbwa na uhaba wa walimu kwasababu ya hatua hiyo ya uhamisho.
Kwa upande wa pili chama cha walimu wa sekondari na vyuo kinaitaka serikali kuwapa walimu silaha ili waweze kujihami panapotokea mashambulizi. Omboko Milemba ni mwenyekiti wa KUPPET na huu ndio wito wake.
Juhudi za kumsaka msemaji wa serikali kuelezea mikakati inayofuatia ziliambulia patupu.Kwenye taarifa yake, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya umeweka bayana kuwa unatiwa wasiwasi na matukio ya kaskazini mwa nchi yanayowahangaisha walimu na watoto wa shule jambo ambalo linakiuka haki za kimataifa.
Chanzo: Thelma Mwadzaya