1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

UN: Yaonya juu ya mgogoro mbaya wa wahamiaji mwaka 2025

6 Desemba 2024

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba viwango vya watu wanaolazimika kuyahama makazi yao vitapanda zaidi mwaka ujao wa 2025, huku chanzo kikubwa kikiwa ni mizozo na majanga mengine.

https://p.dw.com/p/4npQw
Schweiz Genf | UN-Flüchtlingskommissar Filippo Grandi
Picha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Umoja wa Mataifa umesema hali hiyo ya watu kulazimika kuyahama makazi yao inatarajiwa kuwa mbaya kutokana na mizozo na athari za majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanawasukuma watu wengi zaidi kuyakimbia makazi yao.
Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimmbizi, UNHCR Filippo Grandi, amesema katika taarifa yake kwamba shirika hilo, linatafuta dola bilioni 10.25 kwa mwaka ujao, fedha ambazo zitatumika kukabiliana na migogoro inayoongezeka.

Mkutano ulioandaliwa mjini Geneva, Uswisi wa kukusanya ahadi za fedha ulishuhudia serikali na wafadhili wakiahidi dola bilioni 1.14 huku sekta binafsi zikitoa ahadi zilizofikia dola bilioni 1.5. Grandi amesema uthabiti wa kutoa misaada ulioonyeshwa kwa ajili ya wakimbizi na watu wengine waliolazimika kuyahama makazi yao ni ujumbe unaohitajika sana kudhihirisha mshikamano na ubinadamu.

Mizozo na majanga imechangia ongezeko la wakimbizi wa ndani Barani Afrika

Shirika la UNHCR, limesema idadi ya watu wanaolazimika kuyahama makazi yao ni ya kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa wakati ambapo takribani watu milioni 123 wamelazimika kuyahama makazi yao duniani kote. UNHCR imesema idadi ya watu wanaohitaji ulinzi na usaidizi wa shirika hilo inaweza kufikia watu milioni 139 ambao watalazimika kuyakimbia makazi yao ifikapo mwaka ujao 2025.

UNHCR yasema kuna hatari ya migogoro kuongezeka mwaka 2025 

Kongo
Umoja wa Mataifa wasema kuna kuna hatari ya kuongezeka kwa migogoro na majanga ya asili mwaka 2025.Picha: Alain Uaykani/Xinhua News Agency/picture alliance

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi limesema mwaka ujao wa 2025, kuna hatari ya kuongezeka kwa migogoro na majanga ya asili na kwamba migogoro hiyo inatarajiwa kusababisha mateso kwa watu wengi ambao watalazimika kuyahama makazi yao. Grandi aliuambia mkutano wa mjini Geneva kwamba iwapo makubalianao dhaifu ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano nchini Lebanon kati ya Israel na Hezbollah yatakiukwa basi yatasababisha janga kubwa. Mkuu huyo wa UNHCR, pia ameelezea wasiwasi wake juu ya athari zinazoweza kutokea kutokana na kuanza tena kwa mapigano nchini Syria kati ya majeshi ya serikali na vikosi vya waasi. Wakimbizi zaidi ya 400,000 wa Syria waliokuwa Lebanon walivuka na kurejea Syria wakati wa mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.

Mgogoro wa kibinadamu utazidi kuongezea mwaka 2024?

Kulingana na Grandi, pia ana wasiwasi sana na hali ya Sudan, akionya kuwa hakuna mwanga wa kumalizika mgogoro baada ya eneo hilo kukumbwa na vita vinavyoendelea kati ya jeshi la taifa na vikosi vya RSF kwa karibu miezi 20 sasa.
Grandi alisema mapigano hayo yalikuwa yanawaathiri wanawake na watoto "kwa njia za kutisha." Alisema "Ubakaji, ukeketaji, utesaji, kuajiri watoto kwa lazima: kila aina ya unyanyasaji unafanywa huko Darfur."

Grandi pia ameashiria athari kubwa za kibinadamu kutokana na uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine.
Mpango mkubwa wa shirika la UNHCR wa mwaka 2025 ni kwa ajili ya Ukraine iliyopangiwa kupokea dola milioni 550, nchi nyingine zilizomo kwenye orodha ya kupokea misaada ya fedha ni pamoja na Lebanon, Ethiopia, Sudan, Chad, Syria, Jordan, Uganda, Yemen na Sudan Kusini.

Chanzo: AFP