UNHCR: Hali ya misaada ya kiutu ni mbaya mno nchini Ukraine
26 Januari 2024Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa shirika hilo la Kuhudumia Wakimbizi Filippo Grandi, ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani dpa, kwamba mashambulizi ya anga ya Urusi yanayoshuhudiwa kila siku hasa kwenye uwanja wa mapambano na maeneo kadhaa ya mijini, husababisha uharibifu mkubwa ambao huwaathiri raia, ambapo wengi wao hujikuta wakiachwa bila makazi au kulazimika kuyakimbia. Grandi ametoa wito wa kutowasahau raia wa Ukraine:
" Nimeshuhudia uharibifu unaosababishwa na vita, vinavyoendelea kupoteza maisha ya raia. Nyumba kubomolewa, vituo vya afya kushambuliwa, miundombinu kutofanya kazi tena kwa sababu ya vita. Nadhani tofauti kubwa ya mwaka jana na mwaka huu ni kwamba sasa mzozo huu hauangaziwi sana. Kwa namna fulani kuna mwelekeo wa "kujaribu kuzoea" mateso ya watu wa Ukraine. Lakini watu wanaoteseka hawawezi na hawapaswi kuzoea mateso hayo. Hakika hili linanipa wasiwasi na nadhani ni muhimu kumkumbusha kila mtu kwamba nchi hiyo bado iko katikati ya vita vya kikatili na kwamba watu wake daima wanahitaji msaada."
Soma pia: UN yataka dola bilioni 4.2, msaada kwa Ukraine, 2024
Mkuu huyo wa UNHCR alifanya ziara ya wiki nzima nchini Ukraine na kutembelea miradi kadhaa ya utoaji misaada katika mikoa ya Odessa, Kryvyi Rih, Dnipro, Kharkiv na mji mkuu Kiev. Grandi amesema mnamo mwaka 2022 na 2023, shughuli za UNHCR na mashirika mengine ya misaada zilifadhiliwa ipasavyo lakini kumekuwa na tishio la ufadhili huo kusitishwa mwaka huu hasa kutokana na kwamba macho ya ulimwengu yameelekezwa katika mzozo wa Mashariki ya Kati.
Umuhimu wa kukarabati nyumba za raia wa Ukraine
Filippo Grandi amesema kwa sasa, jambo la dharura nchini Ukraine ni kukarabati makazi ya raia na kwamba tangu kuanza kwa mzozo huo Februari mwaka 2022, UNHCR kwa ushirikiano na mashirika mengine ya kiutu, wamefanikiwa kukarabati jumla ya nyumba 27,500. Ameendelea kuwa kufanikisha zoezi hilo, kutasaidia pia wakimbizi kurejea makwao.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu milini 10 nchini Ukraine hawaishi katika makazi yao, huku watu milioni 3.7 wakiwa ni wakimbizi wa ndani huku zaidi milioni 6.3 wakiwa walikimbilia katika nchi nyingine.
Soma pia:Zelensky ahimiza nchi wanachama wa EU na Marekani kuipa Ukraine misaada zaidi ya kifedha
Hayo yakiripotiwa, Urusi na Ukraine wametupiana lawama jana katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ajali ya ndege huko Belgorod ambayo Moscow inadai ilikuwa imewabeba wafungwa wa kivita wapatao 65. Maafisa wa Ukraine wamesema hii leo pia kuwa mashambulizi ya makombora ya Urusi katika mji wa Kharkiv yamesababisha vifo vya watu 11.
Vyanzo: (dpa, afp, ap)