UNICEF: Maelfu ya watoto hawana makaazi mashariki mwa DRC
31 Julai 2022Taarifa mpya ya shirika hilo imeeleza kuwa tangu mwezi Machi mwaka huu, watu zaidi ya 190,000 walilazimika kuvipa kisogo vijiji vyao katika wilaya za Rutshuru na Nyiragongo, ikiongeza kuwa nusu ya idadi hiyo ni watoto.
''Maelfu ya watoto wanakabiliwa na kitisho na hawawezi kupata huduma za msingi ambazo ni muhimu kuwanusuru katika mzozo huu,'' amesema Grant Leaity, Mkurugenzi Mkazi wa UNICEF katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya kufanya ziara katika wilaya ya Rutshuru jana Jumamosi. Wilaya hiyo iko katika Jimbo la Kivu Kaskazini.
Suluhisho bado liko mbali
Leaity aliongeza kuwa yumkini watoto wataendelea kukabiliwa na masaibu hayo, kwa sababu bado watu wana hofu kurejea katika vijiji vyao.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alikutana na watu hao walioyakimbia makaazi yao, walioko katika eneo la Kalengera, ambako wakimbizi wa ndani wanawazidi mara mbili wenyeji.
''Familia za wakimbizi wa ndani zinahitaji msaada wa dharura wa chakula, vifaa vya nyumbani, huduma za afya na maji safi, pamoja na vifaa vya usafi,'' imeeleza UNICEF katika taarifa yake.
Soma zaidi: Rwanda na Congo wakubaliana kusitisha uhasama
Aidha, shirika hilo la msaada kwa watoto limeongeza kuwa wakati mahitaji ya msaada huo yakiongezeka kwa kasi, upatikanaji wake unawasili kwa mwendo wa kujivuta.
''Kutokana na ukosefu wa msaada, baadhi ya watu wanalazimika kurudi katika vijiji vyao, katika maeneo ya mstari wa mbele wa mapigano ambayo sio salama,'' taarifa hiyo ya UNICEF imeonya, na kuongeza kuwa jumuiya ya kimataifa haina budi kuchukua hatua za haraka ili kuepusha madhila zaidi kwa watoto wanaokumbwa na utapiamlo wa kupindukia.
Vurugu mpya za M23
Wilaya ya Rutshuru imejikuta katika hali tete mnamo miezi ya hivi karibuni, kufuatia uwepo wa waasi wa M23 ambao wamekuwa wakipigana na jeshi la serikali ya Kongo.
Soma zaidi: Congo : jopo la wataalamu laamini ungwaji mkono kwa M23
M23 ni vuguvugu linalodhibitiwa na wapiganaji kutoka jamii ya Watutsi ambalo lilisambaratishwa mwaka 2013, lakini lilichukua tena silaha mwaka jana na kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya jeshi la serikali na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, MONUSCO, na limeweza kuyakamata na kuyashikilia maeneo kadhaa.
Serikali ya Kinshasa inaituhumu Kigali kuwaunga mkono waasi hao, tuhuma ambazo Rwanda imezikanusha vikali.
Chanzo: afpe