1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UNRWA: Bidhaa ya mafuta yahitajika haraka Gaza

25 Oktoba 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema ikiwa Israel haitoondoa kizuizi chake kwa bidhaa ya mafuta, basi shughuli zake za msaada katika Ukanda wa Gaza zitasitishwa Alhamisi.

https://p.dw.com/p/4Y1a2
Gaza Leben von Palästinensern im UNRWA-Lager in Khan Yunis
Afisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) akitazama lori la misaada likiwasili huko Khan Yunis-Gaza: 24.10.2023Picha: Ashraf Amr/AA/picture alliance

Tahadhari hiyo imetolewa wakati msafara mwingine wa malori yaliyosheheni bidhaa muhimu kama vile dawa, maziwa ya watoto na maji yakiinga eneo hilo kutokea Misri kwa kupitia kivuko cha Rafah. Siku ya Jumatano, malori 8 kati ya 20 yaliyokuwa yakitarajiwa ndiyo yaliyowasili Gaza.

Tangu Jumamosi, jumla ya malori 62 yamefanikiwa kuingia huko Palestina, idadi ambayo mashirika ya misaada yanasema bado haitoshi kabisa ukilinganisha na mahitaji yaliyopo huko Gaza ambako wanaishi watu zaidi ya milioni 2.

Israel inakataa kuruhusu malori ya mafuta kuingia Gaza , ikisema Hamas inaweza kuyapora mafuta hayo na kuyatumia katika operesheni zake za kijeshi, huku ikisema kuwa kundi hilo la wanamgambo bado limehodhi kiwango kikubwa cha mafuta ambacho wamejilimbikizia wenyewe.

 Wakati vita kati ya Israel na Hamas vikiingia katika siku yake ya 19, Israel imeendeleza mashambulizi yake ya anga huko Gaza huku wanamgambo wa Hamas wakiendelea nao kurusha makombora katika eneo hilo la mpakani.

Gazastreifen | Der Palästinensische Rote Halbmond nimmt am Grenzübergang Rafah Hilfsgüter entgegen
Lori la misaada ya kibinaadamu likiwasili Palestina kupitia kivuko cha Rafah: 24.10.2023Picha: Palestine Red Crescent Society/Handout/REUTERS

Kulingana na wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas, kwa siku ya jana pekee, takriban Wapalestina 700 wameuawa huko Gaza na kwamba tangu kuanza kwa vita hivi Oktoba 7,  zaidi ya watu 6,500 wengi wao wakiwa raia, wameuawa kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limesema jumla ya watoto 2,360 wamefariki dunia kufuatia mashambulizi ya Israel.

Soma pia: Guterres atoa wito wa usitishwaji mapigano Gaza

Ikumbukwe tu kwamba, wanamgambo wa Hamas, ambayo inazingatiwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa kuwa kundi la kigaidi, walivamia na kushambulia kusini mwa Israel na kuua zaidi ya watu 1,400 wengi wao wakiwa raia huku ikiwachukua pia mateka watu wengine zaidi ya 200.

Berlin | Kristalina Georgieva, geschäftsführende Direktorin des Internationalen Währungsfonds
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF Kristalina Georgieva Picha: Britta Pedersen/dpa/picture alliance

Daima kuhusu vita hivyo, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF Kristalina Georgieva amesema vita vinavyopamba moto kati ya Israel na Hamas tayari vimeathiri uchumi wa nchi jirani. Giorgieva ameyasema hayo katika kongamano la wawekezaji wa Saudi Arabia unaofanyika leo hii huko Riyadh na kusisitiza kuwa majirani wa Israel wanahisi madhara ya vita hivyo, hasa wale wanaotegemea utalii.

Mbali na kutoa wito wa usitishwaji mapigano hapo jana katika mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres aliyataja madhila wanayopitia raia wa Palestina:

Wapalestina wamekabiliwa na miaka 56 ya ukaliwaji kimabavu. Wameshuhudia ardhi yao ikiendelea kumegwa na makazi yao kuathiriwa na vurugu, uchumi wao ukidorora, watu wao wakiyahama makazi yao, na nyumba zao kubomolewa. Matumaini yao ya kupata suluhu ya kisiasa kwa masaibu yao, yamekuwa yakitoweka. Lakini malalamiko ya watu wa Palestina hayawezi kuhalalisha mashambulizi ya kutisha ya Hamas. Na pia mashambulizi hayo ya kutisha hayawezi kuhalalisha adhabu ya pamoja ya watu wa Palestina."

Juhudi za kidiplomasia za kuutafutia suluhu mzozo huu

Palästina Emmanuel Macron trifft sich mit Mahmoud Abbas
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akikutana kwa mazungumzo na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas huko Ramallah: 24.10.2023Picha: Ena Christophe/Pool/Abaca/IMAGO

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewasili hii leo mjini Cairo, na amekutana na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi.

Soma pia: Mataifa ya kiarabu yahofia uhamisho mpya wa Wapalestina

Misri imekuwa ikiikosoa Israel kwa kuishambulia kwa mabomu Gaza, ikiishutumu pia kwa kujaribu kuwatimua mamia ya maelfu ya Wapalestina kwenye ardhi yao na kutokomeza hitaji la Wapalestina la kudai kuwa na taifa huru.

Viongozi wa Kiarabu wameshinikiza kusitishwa kwa mapigano na kurejea kwenye mchakato wa kisiasa, na kuonya kuhusu uwezekano wa vita vya Israel na Hamas kupanuka na kuenea katika ukanda mzima.

(DPAE, AFP)