Upinzani DRC wadai Tshisekedi aandaa ushindi wa uchaguzi
11 Januari 2022Wapinzani hao wa Lamuka wanasema ni dhahiri kwamba uchaguzi huo utagubikwa na mivutano hasa kwa kuwaweka wapambe wake wa kisiasa kwenye uongozi wa tume huru ya uchaguzi CENI. Rais Tshisekedi amemteua hivi karibuni mmoja wa wapambe hao kuwa katibu mtendaji mpya wa tume ya uchaguzi.
Katika taarifa iliyochapishwa jana jioni mjini Kinshasa, upinzani unahisi kwamba sio sawa kwa Rais Tishisekedi kumteua kiongozi mpya wa CENI, Denis Kadima ambaye ni mwanachama wa zamani wa chama cha UDPS cha rais huyo na kisha kumteua katibu mpya wa tume hiyo ya uchaguzi, Mabiku Totokani anayechukua nafasi ya Ronsard Malonda kutoka kwenye muungano wa vyama vya FCC vinavyomuunga mkono rais wa zamani Joseph Kabila.
Viongozi wa Lamuka, Martin Fayulu na Adolphe Muzito wanaona uteuzi huo kuwa ushindi wa wazi wa upande wa rais aliyeko madarakani wakihakikisha kuwa ni mtu wake wa karibu, nahivyo upinzani unashuku kwamba uchaguzi wa mwaka ujao utakumbwa na udanganyifu ambao uliandaliwa mapema. Cikuru Mudosa ni katibu mtendaji wa chama cha upinzani cha Ecidé cha Martin Fayulu katika mkoa wa kivu kusini, alisema, "utafiti umeonyesha kwamba bwana Kadima ni mwanamemba wa hama ha UDPS ha bwana Felix. Hata huyo katibu mtendaji naye ni mwanamemba wa UDPS na ndio maana tunaendelea na kuona kama bwana Tshisekedi anaendelea kutayarisha wizi mkubwa sana kwenye uchaguzi, ama hata kama huo uwizi hauwezekani inawezekana hata asitayarishe uchaguzi. Maandamano yataendelea hadi tutakapojikomboa sisi wenyewe."
Kwa hivyo, uongozi wa Lamuka uwataka wananchi wawe makini kuhusu suala hili huku wakisubiri mwito wa kufanya maandamano hivi karibuni mnamo mwezi Februari mwaka huu, na uongozi huo unaitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kuzuia machafuko kwenye uchaguzi wa mwaka ujao wa 2023.
Upande wa chama tawala chaUDPS wanachama wamepuuza lawama hizo za upinzani wakidai kwamba huo ni woga wa wapinzani kabla ya uchaguzi. Edouard Makala ni kiongozi anayehusika na sheria na haki za kibinadamu wa chama cha UDPS mjini Bukavu. Naye alisema "watu wa Lamuka waendelee kuwahamasisha wakaazi kwa ajili ya uchaguzi unaokaribia wa mwaka 2023, waache hayo mambo ya kuingiaingia barabarani, maana wapiga kura hawana haja ya kila siku maamndamano. Wanatakiwa kuwatayarisha wapiga kura kupiga kura vizuri kwenye muhula ujao".
Katika hotuba yake ya hivi karibuni mbele ya wabunge na maseneti mnamo desemba mwaka jana mjini Kinshasa rais Félix Tshisekedi aliahidi kuandaa uchaguzi utakaoheshimu demokrasia katika muda kulingana na katiba ya nchi.
Mitima Delachance, DW, Bukavu.