Upotoshaji mtandaoni wachochea hofu Kenya kuelekea uchaguzi
28 Juni 2022Ripoti ya mwezi huu ya wakfu wa Mozilla, imeangazia machapisho kadhaa kwenye mtandao wa kijamii wa Tiktok yaliyomlinganisha mgombea mmoja wa kisiasa nchini Kenya na Hitler na kudai atashambulia makabila mengine atakapoingia madarakani.
Mwandishi wa ripoti hiyo Odanga Madung, anasema kuwa machapisho hayo yanaongeza hofu katika hali tete ya mazingira ya kisiasa ambayo hapo awali yalishuhudia mapigano mabaya ya baada ya uchaguzi na kuongeza kuwa mitandao ya kijamii inashindwa kukabiliana vilivyo na matumizi mabaya.
Soma pia: IEBC yatoa mafunzo kwa waandishi kuelekea uchaguzi
Madung anasema kuwa matamshi ya chuki yanaweza kuwa magumu kubainisha lakini ni dhahiri kwamba matamshi mengi yana matatizo. Madung ameongeza kuwa hakuna shirika la habari linaloweza kuchapisha hayo nchini Kenya kwasababu ya hatari ya kufungiwa.
TikTok imesema inafanya kazi kuondoa maudhui hatari, na video nyingi zilizoripotiwa na Madung zimeondolewa au kutahadharishwa kuwa nyeti tangu utafiti wake ulipochapishwa.
Hofu ya kuzuka machafuko
Kenya itapiga kura Agosti 9. Uchaguzi mkuu nchini humo mara nyingi huwa na mvutano na wenye mapendeleo
huku wengi wakipiga kura kwa misingi ya kikabila. Wakati mwingine upigaji kura huo hukumbwa na ghasia za kijamii.
Madung alipata zaidi ya video 130 za TikTok zilizo na maudhui ya chuki na upotoshaji katika uchunguzi wa miezi sita, ambazo tayari zilikuwa zimepata maoni zaidi ya milioni 4.
Soma pia: Uidhinishwaji wagombea wa uchaguzi Kenya wakamilika
Mgwili-Sibanda, mkuu wa sera za umma wa App ya Fortune barani Afrika, amesema Tiktok imeandaa timu iliyojitolea kwa uchaguzi huo wa Kenya na pia imekuwa ikitoa habari kuhusu uchaguzi huo.
Katika taarifa, Sibanda amesema kuwa wanapinga na kuondoa habari potofu za uchaguzi, uchochezi wa ghasia na ukiukaji mwingine wa sera zao pamoja na kushirikiana na wakaguzi wa ukweli walioidhinishwa.
Wagombea wakuu wawili wa urais wa Kenya, Naibu Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, wameonyesha imani katika mchakato wa uchaguzi lakini hali bado ni hatari, kulingana na wachambuzi wa kisiasa.
Kulingana na tovuti ya Datareportal, zaidi ya nusu ya idadi ya watu milioni 53 nchini Kenya iko chini ya umri wa miaka 35, na takriban milioni 12 wanatumia mitandao ya kijamii.
Utafiti wa Taasisi ya Reuters mwaka jana uligundua kuwa asilimia 75 ya watumiaji wa habari wa Kenya walipata shida
ya kutofautisha kati ya habari za kweli na za uwongo mtandaoni, na zaidi ya asilimia 60 walisema walikutana na habari za uwongo kuhusu siasa katika wiki iliyopita.
Soma pia:Kalonzo ajiunga tena na kikosi cha Azimio One Kenya
Wakfu wa Mozilla umebainisha kuwa Kenya ambayo mara nyingi hutajwa kuwa Silicon Savannah kutokana na sifa zake za kubobea katika suala la mitandao, pia imeshuhudia kuenea kwa washawishi wengi wa mitandaoni wanaokodishwa kusambaza habari potofu za kisiasa.
Ushawishi wa mitandao ya kijamii
Irungu Houghton, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Amnesty International nchini Kenya, amesema kuwa hawawezi kupuuza ushawishi wa mitandao mikubwa ya kijamii.
Katika mtandao wa Facebook, video moja ilipendekeza kwa uongo kwamba aliyekuwa rais wa Marekani Barrack Obama alikuwa amemuidhinisha mgombea urais Ruto huku mapema mwaka huu, Twitter ilishuhudia hasthtag iliyokuwa ikisambaa na kueneza madai ya uongo dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga.
Soma pia: Juhudi zafanyika kuwazuia mafisadi kugombea nchini Kenya
Machapisho yaliyotambuliwa na Madung kwenye TikTok yalijumuisha video iliyofanyiwa ukarabati iliyoonesha picha ya Ruto akiwa amevalia shati lililokuwa limejaa damu huku akishika kisu, na nukuu iliyodai kuwa ni muuaji. Chapisho hilo lilikuwa na maoni zaidi ya 500,000.
Facebook na Twitter, zimeuambia wakfu wa Reuters kwamba zinachukuwa hatua madhubuti za kukabiliana na habari za kupotosha ikiwa ni pamoja na kuajiri wasimamizi waliobobea na kushirikiana na
wakaguzi huru wa ukweli.
Chanzo: Thomson Reuters Foundation