1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Mashambulizi ya Urusi yauwa wawili Nikopol

Angela Mdungu
9 Mei 2024

Ukraine imesema watu wawili wameuwawa baada ya mashambulizi ya Urusi yaliyoelekezwa katika mji wa kusini mwa nchi hiyo wa Nikopol.

https://p.dw.com/p/4ffOA
Ukraine | madhara baada ya shambulio la Ukraine
Watoa huduma za dharura wa Ukraine katika moja ya maeneo yaliyoshambuliwa na Urusi Picha: Ukrainian Emergency Service/AP/picture alliance

Ukraine imetoa taarifa ya vifo vya watu wawili baada ya mashambulizi ya Urusi mjini Nikopol na kuongeza kuwa, ilifanikiwa kudungua ndege 17 zisizo na rubani kati ya 20 zilizoelekezwa  kwenye eneo hilo.

Soma zaidi: Jeshi la Ukraine ladunguwa droni 13

Mji huo umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na vikosi vya Urusi vilivyojipanga kando ya mto  Dnipro  ambao umekuwa uwanja wa mapambano tangu mwishoni mwa mwaka 2022. Akizungumzia mashambulizi hayo Gavana wa eneo hilo Sergiy Lysak amesema waliouwawa ni mwanamume mwenye miaka 62 na mwanamke wa miaka 65.

Katika tukio jingine, kampuni ya nishati ya Ukraine imeripoti kuwa mitambo miwili ya kuzalisha umeme haifanyi kazi na imepata madhara makubwa baada ya mashambulizi ya Urusi ya mwanzoni mwa juma.

Soma zaidi: Urusi na Ukraine zaendelea kushambuliana kwa ndege za droni

Taarifa ya shirika hilo imesema kuwa kiasi kikubwa cha fedha na juhudi kubwa zitahitajika ili kufanya matengenezo katika mitambo hiyo. Kutokana na uharibifu huo, wizara ya nishati ya Ukraine imesema kuwa inapanga kuongeza mara mbili uingizwaji wa nishati nchini humo.

Shambulio la ndege isiyo na rubani Kharkiv
Moto ukizimwa baada ya shambulio la droni mjini KharkivPicha: Pavlo Pakhomenko/NurPhoto/picture alliance

Mashambulizi ya Ukraine yajeruhi watu 8 Belgorod

Nao maafisa wa jeshi katika mji wa magharibi wa Belgorod, wamesema kuwa watu 8 wamepata majeraha baada ya Ukraine kufanya mashambulizi ya anga usiku kucha. Gavana Vyacheslav Gladkov amelizungumzia pia tukio hilo kupitia ukurasa wake wa jukwaa la Telegram na amefafanua kuwa, majengo kadhaa yakiwemo makazi ya watu na magari yameathiriwa na mashambulizi hayo.

Zaidi Gladkov ameeleza kuwa kwa mujibu wa taarifa za awali, kati ya watu 8 waliojeruhiwa, mmoja ni mtoto wa miaka 11.Majibizano ya mashambulizi kati ya Ukraine na Urusi yanajiri wakati Moscow ikida kuwa vikosi vyake sasa vinavidhibiti vijiji huko Kharkov kaskazini mashariki mwa Ukraine na Avdiivka ulio upande wa mashariki mwa nchi hiyo.

Hata hivyo, jeshi la anga vya Urusi limesema kuwa lilifanikiwa kuyazuia makombora ya kimkakati ya jeshi la Ukraine na  ndege kadhaa zisizo na rubani Jumatano.