Urusi yadai kuukamata mji wa mwisho katika jimbo la Luhansk
3 Julai 2022Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu ndiye ametoa habari hizo akisema vikosi vya nchi yake vimepata ushindi kwenye mji huo wa kimkakati.
Shoigu amemwarifu rais Vladimir Putin wa Urusi kuhusu ushindi huo akisema hatua hiyo inamaanisha sasa Moscow inadhibiti eneo zima la mkoa wa Luhansk.
Hata hivyo msema wa wizara ya ulinzi ya Ukraine Yuriy Sak amesema Lysychansk bado haijachukuliwa kikamilifu na vikosi vya Urusi.
Afisa huyo amenukuliwa akiyasema hayo na shirika la utangazaji la Uingereza, BBC. Amesema hali kwenye mji huo "imekuwa mbaya kwa muda sasa ", akiongeza kwamba vikosi vya Urusi vilivyo kwenye mji huo vinafanya mashambulizi mfululizo.
Sak amegusia ukweli kwamba katika baadhi ya wakati vikosi vya Ukraine vililazimika kusalamu amri kwenye baadhi ya maeneo ili kulinda maisha ya watu lakini iliyakamata tena maeneo hayo baadae. Udhibiti wa jimbo la Donbas - linalojumuisha mikoa ya Luhansk na Donetsk - limekuwa lengo la wazi la Urusi katika uvamizi wake nchini Ukraine.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Urusi amesema hata ikiwa Urusi itaukamata mkoa wa Luhanks bado haitokuwa imelidhibiti jimbo lote la Donbas kwa sababu sehemu kubwa ya mkoa wa Donetsk bado upo mikononi mwa Ukraine.
"Hii ni miji ambayo kwa siku kadhaa imekuwa ikishambuliwa kwa makombora chungunzima, lakini mapambano ya kuwania Donbass bado hayajakwisha" amesema afisa huyo.
Ni vigumu kuthihibitisha kile kinachoendelea kwenye uwanja wa vita
Hata hivyo ni vigumu kubaini upande unaosema kweli kwa sababu ni vigumu kupata taarifa za uhakika kutoka eneo la mapigano.
Taarifa za kukamatwa kwa mji wa Lysychansk zilianza kutangazwa jana na wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoegemea Urusi. Serikali mjini Kyiv ilikanusha habari hizo mara moja.
Hata hivyo mapema siku ya Jumapili, kamanda mmoja wa jeshi la Ukraine alikiri kwamba vikosi vya Urusi vimepata mafanikio zaidi kwenye mapambano ya kuwania mji huo.
Lysychansk, mji uliokuwa na wakaazi zaidi ya 100,000 kabla ya vita, limekuwa eneo la mwisho linaloshikiliwa na vikosi vya Ukraine kwenye mkoa wa Donetsk tangu Urusi ilipoukamata mji wa karibu wa Severodonetsk.
Mapigano bado yamechacha katika vita nchini Ukraine
Kwengineko watu sita wameuwawa leo Jumapili baadaya mji wa Sloviansk ulio mashariki mwa Ukraine kushambuliwa kwa makombora kutoka upande wa Urusi.
Meya wa mji huo Vadym Lyakh amesema hilo ni shambulizi baya kabisa kuulenga mji huo siku za karibuni.
Wakati huo huo watu watatu wameuwawa kutokana milipuko kadhaa iliyotokea katika mji wa Belgorod nchini Urusi karibu na mpaka wa Ukraine.
Moscow imeishutumu Ukraine kwa mfululizo wa mashambulizi dhidi ya mji huo na mikoa mingine inayopakana na Ukraine tangu Urusi ilipoivamia kijeshi Ukraine.
Ukraine haijathibitisha kuhusika na mashambulizi hayo lakini imeyataja kama malipo kwa vitendo vya Urusi kwenye ardhi yake.