1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 18 wauawa kwa makombora ya Urusi nchini Ukraine

1 Julai 2022

Mashambulizi ya makombora ya Urusi kwenye maeneo ya makazi katika mji mmoja karibu na mji wa bandari wa Odesa nchini Ukraine yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 18 wakiwemo watoto wawili .

https://p.dw.com/p/4DW3L
Ukraine-Krieg - Angriff auf Odessa
Picha: Ukrainian Emergency Service/AP Photo/picture alliance/dpa

Video ya shambulio hilo la kabla ya alfajiri ya  Ijumaa  ilionyesha mabaki ya majengo yalioteketea kwa moto katika mji mdogo wa Serhiivka, ulioko kilomita 50 kusini magharibi mwa Odesa. Taarifa za vyombo vya habari vya Ukraine zimesema makombora yalilenga jengo la ghorofa nyingi na eneo moja la mapumziko.

Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema kuwa taifa la kigaidi linawauwa watu wao na kuongeza kuwa kwa kujibu kushindwa kwa taifa hilo katika uwanja wa mapigano, sasa linapigana na raia. Naibu wa ofisi hiyo ya rais Kirill Tymoshenko, amethibitisha kufariki kwa watu hao 18 na watoto wawili. Katika ujumbe kupitia mtandao wa telegram, msemaji wa serikali katika eneo la  Odesa, Serhiy Bartchuk, amesema kuwa watu wengine 30 pia wamejeruhiwa.

Shambulio hilo limetokea siku moja baada ya kuondoka kwa vikosi vya Urusi 

Shambulio hilo linafuatia kuondoka kwa vikosi vya Urusi kutoka kisiwa cha snake siku ya Alhamisi , hatua ambayo ilitarajiwa kupunguza tishio katika eneo la karibu la Odesa. Kisiwa hicho kiko kando ya njia ya meli yenye shughuli nyingi. Urusi ilichukuwa udhibiti wa kisiwa hicho katika siku za mwanzo za uvamizi nchini Ukraine kwa matarajio wazi ya kukitumia kama eneo la kufanya mashambulizi dhidi ya Odesa. Urusi ilionesha kujiondoa kwake kutoka kisiwa hicho cha snake kama 'hatua ya nia njema'.

Jeshi la Ukraine linadai kuwa mashambulizi yake ya silaha na makombora yaliwalazimu wapiganaji wa Urusi kutoroka kwa kutumia maboti mawili ya mwendo kasi. Hata hivyo idadi kamili ya wanajeshi waliondoka haikubainishwa.

Brüssel EU Ukraine Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya - Ursula von der LeyenPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Huku hayo yakijiri, Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Ijumaa ameliambia bunge la Ukraine kwamba uanachama wa Umoja wa Ulaya unaweza kuafikiwa lakini akalitaka kushinikiza mageuzi ya kupambana na ufisadi. Akiwahutubia wabunge hao kwa njia ya video, von der Leyen amewaambia kuwa wameanzisha taasisi za kuridhisha za kupambana na ufisadi lakini zinahitaji kuwa na mamlaka na watu wanaofaa katika nyadhifa kuu.

von der Leyen alisifu bunge na serikali ya Ukraine

Hotuba hiyo ya Von der Leyen ililimwagia  sifa bunge hilo na serikali ya rais Volodymr Zelensky kwa  msukumo wao wa haraka na wenye mafanikio wa kuwa wagombea wa uanachama wa Umoja wa Ulaya. Alisisitiza kwamba makao makuu ya Umoja wa Ulaya na mataifa wanachama wa Umoja huo wanaiunga mkono Ukraine katika mapambanao yake dhidi ya Urusi na ari ya kujiunga na Umoja huo. von der Leyen pia amesisitiza kuhusu haja ya kuendeleza mageuzi ambayo yalianzishwa tangu uasi wa Ukraine wa mwaka 2014 dhidi ya serikali yake ya awali ili kupambana na ufisadi na ubepari katika uchumi wake.