1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yapinga ukomo wa bei kwa mafuta yake

3 Desemba 2022

Urusi imekosoa vikali hatua ya mataifa ya magharibi ya kuweka ukomo wa bei kwa mafuta yake na kutishia kutopeleka nishati hiyo kwenye mataifa yatakayoridhia uamuzi huo.

https://p.dw.com/p/4KRDm
Russland | Tatneft produziert Öl in Tatarstan
Moja ya vituo vya kuchimba mafuta vya Urusi Picha: Yegor Aleyev/TASS/dpa/picture alliance

Australia, Uingereza, Canada, Japan, Marekani na mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya yalitangaza siku ya Ijumaa kuweka ukomo wa bei kwa mafuta ya Urusi wakisema watalipa dola 60 pekee kwa kila pipa.

Ukomo huo wa bei unatarajiwa kuanza kufanya kazi siku ya Jumatatu pamoja na marufuku ya Umoja wa Ulaya dhidi ya kununua mafuta yanaosafirishwa kwa njia ya bahari kutokea Urusi.

Mataifa hayo ambayo ni washirika wa Ukraine yanatumai ukomo kwa bei ya mafuta ya Urusi utaongeza mbinyo kwa mapato ya Moscow yatokanayo na mauzo ya nje ya nishati hiyo na hatimaye kupunguza uwezo wa Urusi kuendelea na vita.

Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin, Dmitry Peskov amesema Urusi inahitaji muda kufanya tathmini ya hatua hiyo ya mataifa ya magharibi kabla ya kutangaza vipi itajibu suala hilo. Hata hivyo imesisitiza kamwe haitokubali mafuta yake kuwekewa ukomo wa bei.

Mwanadiplomasia wa Urusi ayaonya mataifa ya Ulaya dhidi ya kuhujumu mapato ya Urusi

Öltanker Astro Lupus aus Russland
Picha: AP

Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye mashirika kadhaa ya kimataifa huko mjini Vienna, Mikhail Ulyanov, ameonya kwamba mataifa ya Ulaya yatakayounga mkono uamuzi huo yatajutia uamuzi wake.

"Kuanzia mwaka huu, Ulaya itaishi bila mafuta ya Urusi", ameandika Ulyanov kupitia mtandao wa Twitter.

"Moscow imekwishaweka wazi kwamba haitouza mafuta yake kwa nchi zitakazounga mkono ukomo wa bei ambao ni kinyume na bei inayokubalika na soko. Subirini, hivi karibuni Umoja wa Ulaya utaituhumu Urusi kutumia mafuta kama silaha" uliongeza ujumbe wa mwanadiplomasia huyo wa Urusi.

Ukraine yapigia upatu bei ya chini zaidi kwa mafuta ya Urusi

Ukraine |  Wolodymyr Selenskyj
Picha: Ukraine Presidency/ZUMA/IMAGO/ZUMA Wire

Wakati Moscow ikitoa msimamo huo, ofisi ya rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, imeyarai mataifa ya magharibi kuweka ukomo wa bei ya chini kabisa, ikisema ule uliofikiwa na mataifa ya Umoja wa Ulaya na kundi la nchi tajiri la G7 hautoshelezi.

"Itakuwa muhimu kupunguza bei ya pipa hadi dola 30 ili kuuharibu uchumi wa adui haraka," ameandika Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya rais Zelenskyy kupitia ukurasa wa mtandao wa Telegram.

Mtizamo huo wa Ukraine ni sawa na ule uliotolewa na Poland iliyotaka bei ya chini zaidi kwa mafuta ya Urusi. Poland ni miongoni mwa wakosoaji wa mstari wa mbele wa vita vya Urusi nchini Ukraine.

Chini ya makubaliano ya siku ya Ijumaa, kampuni za bima na nyinginezo zinazohitaji kusafirisha mafuta ya Urusi zitapaswa kuchukua yale yanayouzwa kwa bei ya dola 60 kwa pipa au chini ya kiwango hicho.

Sehemu kubwa ya kampuni za bima na usafirishaji mafuta zinaendesha shughuli zake ndani ya Umoja wa Ulaya au Uingereza na zitalazimika kutii ukomo uliowekwa.