Urusi yasema imezidungua droni 42 za Ukraine
22 Desemba 2024Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema leo Jumapili kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga imezidungua droni 42 za Ukraine katika mashambulizi yaliyofanywa usiku wa kuamkia leo katika mikoa yake mitano.
Katika ujumbe uliochapishwa katika mtandao wa Telegram na wizara hiyo ni kwamba droni hizo zilidunguliwa kwenye maeneo ya Oryol, Rostov, Bryansk, Kursk na Krasnodar. Shambulio moja lilisababisha moto katika miundombinu ya mafuta katika kijiji cha Stalnoi Kon, hayo yamesemwa na Andrei Klychkov, Gavana wa mkoa wa Oryol.
Soma zaidi. Russia yaigusa pabaya Ukraine, Kyiv yajibu mapigo
Mashambulizi hayo ya droni ya Ukraine ni ya wiki ya pili mfululizo na yanalenga miundombinu ya mafuta katika maeneo ya Urusi.Hata hivyo wakuu wa mikoa ya Urusi ya Rostov na Bryansk wamesema hakuna majeruhi au uharibifu mkubwa uliosababishwa na mashambulizi hayo ya hivi karibuni.