Urusi yasema luteka za nyuklia ni salama
18 Februari 2022Urusi na Magharibi zinavutana kufuatia hali ya wasiwasi iliyoibuka kutokana na madai dhidi ya taifa hilo kwamba inataka kuivamia Ukraine. Urusi inasema hayo wakati mkutano wa kilele wa usalama unaoupatia kipaumbele mvutano huo ukifunguliwa mjini Munich Ujerumani, lakini taifa hilo likiwa halijapeleka mwakilishi wake hata mmoja.
Soma Zaidi:Mzozo wa Ukraine: Juhudi za kidiplomasia zaendelea
Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema luteka za kijeshi hufanyika katika misingi ya kawaida tu na hata hizo za nyuklia pia hufanyika baada ya taarifa kusambazwa huku na kule kupitia njia za kidiplomasia. Amesema hii haitakiwi kuibua wasiwasi na maswali kwa sababu kila mmoja aliarifiwa mapema.
Rais Vladimir Putin wa Urusi ataongoza mazoezi hayo akiwa katika chumba maalumu maarufu Situation room, amesema Peskov, ingawa hakuelezea zaidi ni wapi hasa. Amesema mazoezi hayo ya nyuklia hayawezi kufanyika bila ya kuwepo mkuu wa nchi.
Amesema ''Putin atakuwepo kwenye chumba maalumu. Majaribio kama haya ya kufyatua makombora huwa hayafanyiki bila ya mkuu wa nchi kuwepo. Kama mnavyojua mambo ya kisanduku cheusi, kitufe chekundu na mengineyo na mengineyo. Ni kwa namna gani shughuli hiyo itafanyika, hii si taarifa ya kutolewa kwa umma.''
Na huko Munich nchini Ujerumani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema huenda huu ndio wakati hatari zaidi kwa ulimwengu kuliko hata enzi ya Vita Baridi. Guterres ameonya kwamba kosa dogo tu kati ya mataifa yenye nguvu linaweza kusababisha janga kubwa kabisa.
Soma Zaidi: NATO yajitayarisha kupambana na kitisho cha Urusi Ukraine
Urusi yasusia mkutano huo. Ujerumani yasema imekosa fursa adimu.
Amekiri katika mkutano huo wa kilele wa usalama kwamba, kitisho cha kiusalama ulimwenguni kwa sasa ni kigumu mno na pengine ni cha juu zaidi kuliko wakati huo uliopita, huku akiziomba pande zinazovutana kuwa waangalifu mno na matamshi yao.
Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris, waziri wa mambo ya kigeni Anthony Blinken na rais wa Ukraine, Vilodymyr Zelensky wanahudhuria mkutano huo, lakini hakukuwa na afisa yeyote mwandamizi kutoka Urusi. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema Urusi imeikosa fursa hiyo na hasa wakati huu ambapo kitisho ni kikubwa.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amewaambia waandishi wa habari kwenye mkutano huo kwamba hali inasalia kuwa tete nchini Ukraine, wakati waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine wakisema wanajiandaa kuwaondoa wakazi wao na kuwapeleka Urusi. Muda mfupi uliopita, rais Putin aliiambia Ukraine kuzungumza na waasi hao inaowaunga mkono, akiangazia ongezeko la hofu ya kikanda na kutoa mwito wa utekezwaji wa mchakato wa amani wa Minsk.
Waziri wa ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin amesema akiwa Warsaw, Poland kwamba bado milango ya diplomasia iko wazi, ingawa taifa hilo liko mbioni kuongeza wanajeshi karibu 4,700 kuungana na wenzao wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO huko Poland.
Mashirika: AFPE/APE/RTRE