Urusi yazidisha mashambulizi katika mji wa Avdiivka
10 Novemba 2023
Rais Vladimir Putin amefanya ziara ya kushtukiza usiku wa kuamkia leo katika makao makuu ya jeshi huko Rostov-on-Don, eneo linalotumiwa na Moscow kuratibu vita nchini Ukraine.
Ikulu ya Urusi Kremlin imetoa taarifa ya ziara hiyo ya Putin leo Ijumaa na hii ikiwa ni ya pili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja huko Rostov-on-Don . Rais huyo wa Urusi ametembelea eneo hilo baada ya kumaliza hapo jana ziara yake rasmi nchini Kazakhstan, na aliandamana na Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu na kamanda wa operesheni za kijeshi nchini Ukraine, Valery Gerasimov.
Putin ambaye mara ya mwisho ameitembelea Rostov-on-Don mwishoni mwa mwezi Oktoba, ameonyeshwa zana mpya za kijeshi na kufahamishwa maendeleo ya kile Moscow inakiita "operesheni maalum ya kijeshi" nchini Ukraine.
Matokeo katika uwanja wa mapambano
Urusi imeendeleza mashambulizi yake nchini Ukraine, na vikosi vyake vimezidisha mashambulizi hayo katika mji wa mashariki wa Avdiivka. Afisa mwandamizi wa Ukraine amesema jeshi la Ukraine limefanikiwa kuyazima mashambulio mengi ya Urusi.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amepongeza mashambulizi ya kujihami ya Ukraine yaliyoanzishwa mwezi Juni na kusema yanatoa "mwamko" bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.
Soma pia: Zelensky: Vita vya Ukraine katika eneo la Bahari Nyeusi vitaingia katika historia
Vikosi vya Urusi vimejikita katika maeneo ya mashariki mwa Ukraine ya Donetsk na Luhansk tangu viliposhindwa kuudhibiti mji mkuu Kyiv katika siku za kwanza za uvamizi wao Februari mwaka jana. Tangu katikati ya mwezi Oktoba wanajeshi wa Moscow wamekuwa wakizidisha mashambulizi kwenye mji ulioathirika pakubwa wa Avdiivka, ukiwa kama lango la kuingia katika mji wa Donetsk, takriban kilomita 20 kutoka upande wa mashariki.
Katika hatua nyingine Mamlaka ya Ulinzi wa anga ya Urusi imesema imedungua mapema leo ndege mbili zisizo na rubani za Ukraine katika rasi ya Crimea na nyingine moja katika mkoa wa Tula kusini mwa mji mkuu Moscow. Hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa na shirika la habari la Urusi RIA likinukuu tamko la wizara ya ulinzi ya Urusi.
Soma pia: Ukraine yakabiliana na mashambulizi ya Urusi huko Avdiivka
Hayo yakijiri, Ukraine inadhamiria Februari mwaka ujao kufanya mkutano wa kilele utakao waleta pamoja viongozi wa mataifa mbalimbali duniani, ili kujaribu kujenga muungano wa kimataifa utakaosaidia kuidhinisha "mapendekezo" ya Rais Zelensky ili kurejesha amani nchini Ukraine.
Lakini Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa serikali mjini Kyiv amesema mkutano huo wa kilele wa amani kwa ajili ya Ukraine unafifishwa na mzozo unaoendelea huko Gaza na hivyo kutatiza azma ya Ukraine ya kupata uungwaji mkono wa kidiplomasia kwenye ngazi ya kimataifa.