1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utulivu warejea Kenya baada ya siku ya maadamano

Thelma Mwadzaya16 Julai 2024

Hali ya kawaida inaanza kurejea baada ya maandamano kufanyika kwenye miji kadhaa kote nchini Kenya kushinikiza uwajibikaji na kuwakumbuka waliouawa.

https://p.dw.com/p/4iNeF
Maandamano Kenya
Watu kadhaa walikamatwa katika maandamano ya kudai uwajibikaji serikalini kote KenyaPicha: KABIR DHANJI/AFP/Getty Images

Kufikia sasa, tume ya taifa ya kutetea haki za binadamu, KNCHR, inakadiria watu 50 kuuawa na wengine 59 kukamatwa au kutoweka tangu maandamano hayo kuzuka.

Kutwa nzima, maandamano ya amani ya kushinikiza uwajibikaji na kuwakumbuka waliouawa yamefanyika kwenye miji kadhaa kote nchini Kenya. Jijini Nairobi, moshi na ukungu ulitanda baada ya maafisa wa usalama kuwarushia waandamanaji makopo ya gesi ya kutoa machozi.

Maandamano Kenya
Waandamanaji wanashinikiza uwajibikaji serikalini na kusimama na wenzao waliouawa katika maandamanoPicha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Hekaheka zilishuhudiwa mtaani Mlolongo katika kaunti jirani ya Machakos ambako maafisa wa kutuliza ghasia ya GSU walilazimika kuingilia kati kutuliza hali.

Mjini Karatina katika kaunti ya Nyeri, wakaazi walijitokeza kuishinikiza serikali kuwajibika mintarafu waliouawa kwenye maandamano ya wiki tatu zilizopita ya kupinga mswada wa fedha wa 2024 uliotupwa nje. Waaandamanaji waliwasha moto barabarani na kuimba nyimbo. Inadaiwa polisi waliwafyatulia risasi ila haikuthibitika kama zilikuwa za moto au la. Biashara na maduka yalifungwa kutwa nzima.

Soma pia: Rais wa Kenya avunja baraza lake la mawaziri baada ya wiki kadhaa za maandamano

Huko Kaunti ya Nakuru, siku ilianza kimya kisha mambo yakabadilika baadaye.Waandamanaji walidai kuwa walidumisha amani ila walihangaishwa na maafisa wa usalama.

Rais William Ruto avunja baraza lake la mawaziri

Mjini Kisumu maandamano yalianzia kwenye kituo kikuu cha basi na wakaazi walielekea katikati ya jiji wakiimba nyimbo za uzalendo. Kinyume na ilivyotarajiwa mtaa wa Kondele haukuwa kitovu cha maandamano ya leo. Maafisa wa polisi waliwatazama kwa mbali waandamanaji hao waliojiunga na waendesha pikipiki maarufu boda boda.

Wakati huohuo, tume ya taifa ya kutetea haki za binadamu, KNCHR, imechapisha takwimu za waliouawa tangu maandamano ya kudai uongozi bora kuanza wiki nne iliyopita. Takwimu zinaeleza kuwa 50 wamepoteza maisha yao na wengine 59 ima wamekamatwa au kutoweka. Mwanzoni mwa wiki hii, maiti zisizopungua 8 zilizopatikana kwenye magunia ziliopolewa timboni Kware mtaani Embakasi jijini Nairobi.

Miili yapatikana kwenye dampo Nairobi
Miili ilipatikana kwenye magunia katika dampo moja viungani mwa NairobiPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Shughuli ya kuzikagua imeahirishwa hadi kesho Jumatano. Mshukiwa mkuu aliyefikishwa mahakamani asubuhi sasa anazuiliwa. Idara ya upelelezi nchini Kenya, DCI, inaendelea kufuatilia kesi hiyo kwani mshukiwa huyo alikiri kuwaua wanawake 42 tangu mwaka 2022 akiwemo mkewe Imeda Judith Halenya.

Kwa upande mwengine, wakfu wa Ford wa Marekani umekanusha madai kwamba unafadhili maandamano yanayoendelea nchini Kenya. Taarifa hiyo imetolewa baada ya rais William Ruto kuunyoshea wakfu huo wa Ford kidole cha lawama. Kwa upande wake, wizara ya usalama wa taifa inasisitiza kuwa iko chonjo kulinda maisha ya wakenya ila wahalifu hawatapewa nafasi.