1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utumwa bado upo hata nchini Ujerumani

23 Agosti 2018

Leo ni siku ya kimataifa ya kutanabahisha juu ya kuendelea kuwepo biashara ya utumwa. Licha ya kupigwa marufuku, udhalimu huo bado upo katika sehemu mbalimbali za dunia ikiwa pamoja na nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/33cH8
Griechenland Demonstration gegen Menschenhandel in Athen
Picha: Louisa Gouliamaki/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa makadirio ya shirika la Australia la kupambana na utumwa duniani, linaloitwa "Walk Free Foundation", wapo watu zaidi ya milioni 40 wanaoishi katika utumwa mambo leo duniani, na miongoni mwa hao 167,000  wapo nchini Ujerumani. Idadi hiyo inawakilisha takriban asilimia 0.2 ya watu wote nchini ujerumani. Tofauti na utumwa wa hapo zamani, ujakazi uliopo sasa katika sehemu mbalimbali za dunia unajitokeza vingine kabisa. Mwanzilishi mwenza wa shirika hilo bi. Grace Forrest amesema lengo la shirika lake ni kuhakikisha kwamba biashara zote duniani zinatoa kipaumbele katika suala la kukabiliana na utumwa mambo leo.

Kwa mujibu wa maelezo ya asasi ya kupambana na utumwa,ya "Walk Free Foundation",utumwa ni hali ya kutumikishwa inayomfika binadamu ambapo hawezi kuondokana nayokutokana na kutishwa, kulazimishwa, kudanganywa na kubanwa kwa mabavu. Utumwa mamboleo unaendelea katika namna mbalimbali kwa mfano katika biashara ya kuwauza binadamu au kwa njia ya madeni yanayowaelemea watu.

Biashara ya kuwauza binadamu haifanyiki katika nchi kama Libya tu, au Qatar na katika Jamhuri ya Kideomkrasia ya Kongo ambako udhalimu huo hufichuliwa mara kwa mara katika vyombo vya habari. Uovu huo uko pia barani Ulaya. Baraza la Ulaya lilitanabahisha mnamo mwezi wa Aprili kwamba biashara ya kuuza binadamu na utumwa mamboleo ni maovu yanayoendelea kutendeka barani humo. Watu bado wanaendelea kudhulumiwa na kutumiwa kama nguvu kazi kwa bei rahisi!

Waandamanaji wamebeba mabango yanayohimiza juu ya kuumaliza utumwa
Waandamanaji wamebeba mabango yanayohimiza juu ya kuumaliza utumwa Picha: Getty Images/P. Macdiarmid

Kwa mujibu wa idara kuu ya Ujerumani ya kupambana na uhalifu, BKA, hapa nchini Ujerumani ni wahamiaji wanaoathirika na utumwa mambo leo na hasa katika sekta ya ujenzi na mahotelini.  Wahamiaji pia wanatumikishwa majumbani na katika sekta za kilimo, machinjioni na katika sekta ya usafirishaji. Mwaka jana pekee kesi zilizowahusu wahamiaji 180 zilisikilizwa mahakamani, idadi kubwa miongoni mwa watu hao walitoka Ulaya ya mashariki. Utumwa mamboleo ulioenea nchini Ujerumani ni ule unaohusu watu kuuzwa ili kuridhisha haja za kingono za watu wengine.

Mwenyekiti wa shirika la kimataifa, kutetea haki ICJ tawi la Ujerumani Dietmar Roller amesema utumwa mamboleo bado unasuasua kama kinyonga na unaendelea kwa kujificha.

Ndiyo sababu Ujerumani inaitwa kuwa ni danguro la barani Ulaya, kama asemavyo mwenyekiti huyo wa shirika la kimataifa la kutetea haki Dietmar Roller. Kwa mujibu wa taarifa ya idara kuu ya kupambana na uhalifu BKA mwaka uliopita zilifanyika kesi 327 mahakamani na kwa jumla watu 500 waliorodheshwa kuwa ni makahaba. Katika sekta ya ujenzi wanaotumikishwa ni wanaume na katika udhalilishaji wa kingono wanaoathirika aghalabu ni wanawake kutoka nchi za Ulaya Mashariki.

Utumwa mambo leo mwananmke aliyetumbukizwa kwenye biashara ya ngono barani Ulaya
Utumwa mambo leo mwananmke aliyetumbukizwa kwenye biashara ya ngono barani UlayaPicha: picture-alliance/PA Wire/D. Lipinski

Wakati huo huo, idara inayopambana na uhalifu huo nchini Ujerumani imefahamisha kwamba idadi ya wanawake kutoka Nigeria wanaotumikishwa kama makahaba hapa nchini imeongezeka. Hata hivyo juhudi zinafanyika kupambana na hali hiyo. Katika miaka ya hivi karibuni wahalifu wameendelea kumulikwa kwa ukaribu zaidi. Polisi wanawakamata wahalifu kati ya 50 na 60 kila mwaka hapa nchini Ujerumani.

Lakini mwenyekiti wa tawi la Ujerumani la shirika la kimataifa la kutetea haki, ICJ, Bwana Roller amesema idadi sahihi ya watu wanaowatumikisha wanawake kwenye madanguro nchini Ujerumani haifahamiki, lakini mwenyekiti huyo amesema juhudi zaidi zinapaswa kufanyika ili kupambana na  uhalifu huo.

Mwandishi: Zainab Aziz/Ines Eisele/DW

Mhariri: Grace Patricia Kabogo